1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS kutuma ujumbe wa kijeshi nchini Guinea-Bissau

4 Februari 2022

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS wamekubaliana kutuma wanajeshi nchini Guinea Bissau kulisaidia taifa hilo kurejesha uthabiti kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa mapema wiki hii

https://p.dw.com/p/46W3J
Ghana Accra | Economic Community of West African States | ECOWAS
Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Uamuzi huo umefikiwa wakati wa mkutano wa viongozi wa kanda ya ECOWAS yenye wanachama 15 uliofanyika jana mjini Accra nchini Ghana. Hata hivyo taarifa iliyotolewa haikueleza kwa undani hasa ni lini na hata idadi ya wanajeshi watakaopelekwa Guinea Bissau.

ECOWAS ilikwishawahi kutuma ujumbe kama huo wa kijeshi nchini Guinea Bissau kuanzia mwaka 2012 hadi 2020 baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi.

Dhima yake ilikuwa ni kuwazuia wanajeshi kuingilia siasa za nchi hiyo na kuwalinda viongozi wa kisiasa.

Uamuzi huo wa ECOWAS yumkini umechochewa na taarifa ya serikali ya Guinea Bissau iliyosema jaribio la mapinduzi la siku ya Jumanne wiki hii lilipangwa kwa ustadi mkubwa na inaonesha lilifadhiliwa vizuri.

Inaarifiwa lengo la washambuliaji waliojihami kwa silaha nzito lilikuwa ni kumuua rais Umaro Sissoco Embalo na viongozi wote wakuu wa serikali na kisha kutwaa madaraka.

ECOWAS yakaza uzi tawala za kijeshi 

Umaro Sissoco Embaló und Offiziere der Armee
Picha: Präsidentschaft der Republik Guinea-Bissau

Jaribio la mapinduzi nchini Guinea Bissau lilikuwa tukio jingine la karibuni kabisa kwenye kanda ya Afrika Magharibi ambayo inaandamwa na visa vya wanajeshi kuziondoa kwa nguvu madarakani serikali za kiraia.

Jumuiya ya ECOWAS imejitwika dhima kubwa kwa kuyachukulia hatua nzito mataifa yalifanya mapinduzi na imerejea msimamo wake wa kupinga wanajeshi kutwaa madaraka.

Jean-Claude Kassi Brou ni rais wa Halmshauri Kuu ya Jumuiya ya ECOWAS na amesema "Hali hii, hali ya usalama siyo sababu ya jeshi kuchukua madaraka. Kazi ya jeshi ni kulinda mipaka na kupambana na shughuli za kigaidi. Kwa sababu taathira za mapinduzi haya ni kupungua kwa uungaji mkono wa jumuiya za kikanda na kimataifa hususan katika mapambano dhidi ya ugaidi"

Hadi sasa ECOWAS imesitisha uanachama wa mataifa matatu ya Mali, Guinea na Burkina Fasso kutokana na mapinduzi.

Mali na Guinea yaonja hasira za ECOWAS 

Katika mkutano huo wa jana viongozi wa kanda hiyo walijizuia kuiwekea vikwazo Burkina Fasso na badala yake kuwataka watawala wa kijeshi kutangaza tarehe rasmi ya kurejea kwa utawala wa kiraia.

Infografik Putsche in ECOWAS Staaten seit 2020 DE

Kadhilika imetaka kuachiwa huru kwa viongozi wote wa kisiasa wanaoshikiliwa ikiwemo rais Roch Christian Kabore.

Ingawa ECOWAS imetishia kuichukulia vikwazo Burkina Fasso iwapo wanajeshi hawatarejesha utawala wa kiraia, hatua kama hizo hazijafanikiwa sana kwa mataifa ya Mali na Guinea.

Licha ya juhudi za kutaka kurejeshwa utawala wa kiraia nchini Mali, watawala wa kijeshi walipuuza ratiba ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia mwezi huu na badala yake  wamependekeza mchakato huo kuchukua hadi miaka mitanoo.

Uamuzi huo ulijibiwa vikali na ECOWAS iliyotangaza vikwazo dhidi ya Mali ikiwemo kufunga mipaka ya nchi zake na taifa hilo lenye mzozo.

Hatma ya kurejea utawala wa kiraia nchini Guinea nayo bado inajikokota. ECOWAS hapo jana ilitangaza vikwazo ziada kwa mataifa hayo mawili ikiwemo dhidi ya viongozi wa kijeshi na familia zao.