1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ecosia yapambana na uchafuzi wa mazingira

Admin.WagnerD8 Novemba 2010

Harakati za maisha yetu zinachangia kwa kiasi kikubwa kuchafua mazingira, si kupitia vyombo vya usaifri tu, bali hata mitandao ya kompyuta. Lakini sasa wataalamu wamevumbua njia ya kutunza mazingira mtandaoni, Ecosia

https://p.dw.com/p/Q1mt
Christian Kroll, mwanzilishi wa Ecosia
Christian Kroll, mwanzilishi wa EcosiaPicha: Christian Kroll

Kila mtu anaingia kwenye kiboksi cha kutafutia taarifa cha mtandao wa Google na akabonyeza kitufe cha "Enter", huwa tayari ameshaongeza hewa chafu ya Kabonidioksidi katika tabaka hewa. Sophie Fabricius, mtaalamu wa uhusiano baina ya matumizi ya kompyuta, anafanya kazi katika taasisi inayojihusisha na upambanaji wa hewa hii kwa njia ya mtandao.

Akizungumzia namna utumiaji wa injini za kutafutia taarifa kwenye mtandao unavyoharibu mazingira, anasema kwamba injini kubwa za kutafutia taarifa hizo zinaendeshwa na sava kubwa. Ili ziweze kufanya kazi, sava hizi hutumia kiwango kikubwa cha umeme na hivyo huzalisha kabonidioksidi. Sava nyingi haziendeshwi kwa nishati jadidifu, na kwa hivyo zinatumia kiwango kikubwa cha nishati za visukuku, ambazo zenyewe zinazalisha kiwango kikubwa cha kabonidioksidi.

Sura ya injini ya kutafutia taarifa mtandaoni, ecosia.org
Sura ya injini ya kutafutia taarifa mtandaoni, ecosia.orgPicha: Screenshot Ecosia.org

Ni kwa sababu hii, ndipo Christian Kroll, kijana wa Kijerumani mwenye miaka 26, alipovumbua injini ya kutafutia taarifa kwenye mtandao ambayo ni rafiki kwa mazingira. Inaitwa Ecosia au Google ya Kijani, ambayo kwa sasa ipo kwa lugha za Kijerumani, Kiingereza, Kihispania, Kifaransa, Kitaliano na Kidachi. Ecosia inatumia teknolojia ya Yahoo na Bing kukusanyia taarifa na inapata fedha zake kupitia ruhusa inazotoa kwa kutumiwa taarifa hizo kwa wanaozihitaji, wafadhili na matangazo. Kwa mfano, kila mtu anapofungua tangazo lolote, mitandao ya Yahoo, Bing na Ecosia hulipwa.

Sehemu moja ya fedha inazopata Ecosia huenda kwenye uendeshaji wa ofisi na malipo kwa wafanyakazi wake watano wa kujitolea. Sehemu iliyobakia, ambayo huwa karibuni euro 130,000, inakwenda kwa Wakfu wa Kimataifa wa Ulinzi wa Mazingira, WWF, nchini Brazil, kwa ajili ya mradi wa kuutunza msitu wa asili wa Amazon. Kwa kufanya hivi, Ecosia inajaribu kuifidia ile nishati iliyotumika kwenye injini yake kutafutia taarifa.

Mkuu wa mradi huo, Christian Pläp, anasema kwamba wanafurahishwa sana na fedha hizi, maana zinapatikana kwa wakati na kwa ukamilifu.

"Kwa kweli tumetiwa moyo sana na ushirikiano huu. Unapofikiria kwamba unaweza kufanya nini na euro 130,000, bila ya shaka ni nyingi. Kwazo tunaweza kufadhili elimu ya ulinzi wa mazingira, kwa wafanyakazi wetu na kwa wenyeji wa hapa, na mengine kadhaa. Hizi pesa nyingi kuzipata kwa pamoja. Hakuna mtu anayeweza kutupa fedha nyingi kama hizi kwa ajili ya ulinzi wa mazingira. Hilo ni sahihi kabisa." Anamalizia Pläp

Mwandishi: Mohammed Khelef/Nicolas Martin/ZPR

Mhariri: Josephat Charo