1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola: Mambo unayotakiwa kuyajua

17 Februari 2021

Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari zimetangaza kuwa na maambukizi ya homa ya Ebola. Hali hii inarejea tena baada ya homa hiyo iliyoathiri afya na kugharimu maisha ya watu kutangazwa kumalizika.

https://p.dw.com/p/3pSjM
Liberia Händewaschen gegen Ebola
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Miaka mitano baada ya Guinea kutangazwa kuwa haina Ebola sasa imetangaza tena kuwa ugonjwa huo ni "hali ya janga." Maafisa wameahidi kushughulikia haraka janga hilo, na hiki hapa ndicho unachotakiwa kukijua kuhusu homa hiyo ya Ebola.

Guinea imetangaza kuibuka upya kwa Ebola baada ya visa saba kuthibitishwa na lakini pia angalau vifo vitatu.

Katika eneo ambako hapo awali kulikuwa kitovu cha mlipuko mbaya zaidi wa Ebola ulimwenguni, kuibuka upya kwa visa vya homa hiyo kunaashiria kurejea tena kwa maradhi hayo ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 11,300 wakati ilipozuka kati ya mwaka 2013-2016.

Soma Zaidi: Visa vya Ebola vimeongezeka magharibi mwa Afrika

Ingawa janga la COVID-19 limechangia kuwepo na upungufu wa upatikanaji wa rasilimali za afya, shirika la afya ulimwenguni, WHO mara moja lilipeleka chanjo nchini Guinea ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa mlipuko huo, pamoja na kuandaa vipimo, kufuatilia historia ya maambukizi lakini pia vituo vya kuwatibu wagonjwa.

Mlipuko ulianzaje?

Ebola Guinea Fieber Messung
Mtumishi wa afya akiwapima joto raia katika mji mkuu wa Guinea, ConakryPicha: picture-alliance/AP Photo/Y.Bah

Kiini hasa cha maradhi hayo bado haijajulikana, lakini maafisa wa afya wa Guinea wamefuatilia mlipuko huo kuanzia kwenye shughuli ya mazisho ya muuguzi mmoja mwanzoni mwa mwezi Februari katika mji wa Goueke, karibu na mji ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo wa Nzerekore.

Visa vyote saba vilivyogunduliwa vilianzia kwenye mazishi hayo baada ya kuripotiwa dalili za kuharisha, kutapika na kutoka damu. Angalau watu watatu tayari wamefariki dunia na wengine bado wako hospitalini.

Tamaduni za mazishi huko Afrika Magharibi, ambako watu huosha maiti ambazo mara nyingine huenda zimeathiriwa na virusi vya Ebola, huko nyuma zilionekana kama zinazochangia zaidi kusambaza maradhi y Ebola. Mtu ananweza kukaa na virusi vya Ebola kuanzia siku mbili hadi wiki tatu ili kuanza kuonyesha dalili.

Mlipuko huo wa Guinea, unafuatia ule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo tayari kumethibitishwa vifo kadhaa ikiwa ni miezi mitatu tangu taifa hilo la Afrika ya Kati kutangaza kumaliza janga hilo mwezi Novemba, 2020 lililosababisha vifo vya watu 55 kati ya visa 130.

Soma Zaidi: UN: Itachukua muda mrefu kuidhibiti Ebola

Visa vya Guinea na Congo havidhaniwi kuwa na mahusiano.

Ebola ni nini?

Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binaadamu baada ya majimaji yaliyoko kwenye miili yao, damu ama viungo vyao kugusana, lakini pia unaweza kuambukizwa kwa kukaa kwenye eneo lililoathiriwa.

Watu wanaoambukizwa hupata homa, maumivu ya misuli, vidonda vya kooni, kuharisha, kutapika na kutoka damu ndani na nje ya mwili. Kwa kawaida hufariki dunia kutokana na upungufu wa maji mwilini ama baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi. Ni ugnojwa unaoambukuzwa kwa haraka, na kusababisha idadi kubwa ya vifo. Lakini tofauti na virusi vya corona, wagonjwa hupata dalili za haraka, hivyo kufanya mazingira ya ufuatiliaji kuwa mepesi.

Guinea Ebola in Dubreka
Watumishi wa afya wakimsaidia mgonjwa wa Ebola nchini GuineaPicha: K. Tribouillard/AFP/Getty Images

Chanjo ipi inaweza kusaidia?

Baadhi ya chanjo zilitengenezwa na kujaribiwa ili kukabiliana na janga hilo la Ebola kati ya mwaka 2014 na 2016. Nyingine zilionyesha mafanikio na kutumika kulidhibiti huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Cong. Chanjo inayotumika zaidi ni ya Ervebo inayotengenezwa na kampuni ya Merck, na hutolewa dozi moja tu. Kwa mara ya kwanza ilijaribiwa Guinea mwaka 2015 na kiasi cha watu 16,000 walichanjwa na 350,000 walipewa chanjo hiyo nchini DRC.

Chanjo nyingine iliyoidhinishwa ni ya Johnson&Johnson ambayo hutolewa mara mbili, siku 56 baada ya dozi ya kwanza.

Shirika la afya WHO limesema kupitia mwakilishi wake nchini Guinea, Alfred George Ki-Zerbo kwamba wako tayari na wanawasiliann na wazalishaji ili kuhakikisha chanjo muhimu zinapatikana haraka iwezekanavyo.

Nini kifanyike kuudhibiti?

Wataalamu wanasema, udhibiti ndio njia kuu ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Sababu moja ya milipuko iliyopita kuwa mibaya zaidi na kudumu kwa muda mrefu ilikuwa ni kwa sababu haikugunduliwa haraka na watumishi wa afya walivyoushughulikia taratibu, tofauti na sasa. Mataifa jirani ya Liberia na Sierra Leone, tayari yamejiweka katika tahadhari ili kujilinda.

Tamaduni za mazishi na ulaji wa nyama za porini vimeendelea kutiliwa shaka linapokuja suala la namna bora zaidi ya kuepukana na maambukizi ya Ebola. Tafiti za awali zinaonyesha kuzuiwa kwa nyama za porini kama mkakati wa kujizuia na Ebola inaweza ikachochea jamii kutoamini tafiti za kiafya.  

Wataalam wanaonya kuwa kuongezeka kwa uvamizi katika makazi ya wanyamapori kunazidi kuongeza hatari ya maambukizi, kama ulimwengu ulivyoshuhudia na janga la virusi vya corona.

Mashirika: DW