1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EAC yazuwia shughuli zake kwa kuhofia corona

16 Machi 2020

Jumuiya ya Afrika Mashariki imetangaza kusitisha mikutano yote iliyopangwa kufanyika katika ofisi zake zilizopo Arusha kaskazini mwa Tanzania, kufutaia hofu ya maambukizi ya virusi vya corona iliyotanda kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/3ZW1d
East African Community Gipfel Tansania Arusha
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Tamko la Jumuiya hiyo linakuja katika wakati ambapo mkoa wa Arusha, yaliko makao makuu ya Jumuiya, kwa sasa unachukua tahadhari kubwa ya kujikinga na virusi hivyo baada ya kuripotiwa kwa visa kadhaa vya maambukizi katika nchi jirani ya Kenya, unayopakana nayo.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Vicent Biruta, amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Liberat Mfumukeko, ya kusitisha mikutano yote inayojumuisha mikusanyiko mikubwa ya watu kutokana na hofu ya virusi vya COVID-19.

Taarifa hiyo inafafanua kwamba miongoni mwa mikutano iliyopangwa kufanyika hivi karibuni ni pamoja na mkutano wa 21 wa marais wa nchi wanachama uliokuwa ufanyika Jumatatu (16 Machi), huku mikutano mingine ikipangwa kufanyika kwa njia ya video.

Infografik Verlauf der COVID-19-Epedemie 16.3.2020 EN
Mchoro unaoonesha hali ya maambukizi na vifo kutokana na kirusi cha corona duniani kufikia tarehe 12 Machi 2020.

Mpaka wa Namanga waimarisha ukaguzi

Katika hatua nyingine, tahadhari zaidi zimeendelea kuchukuliwa katika mpaka wa Namanga unaoziunganisha nchi za Kenya na Tanzania kufuatia visa vitatu vya corona kuripotiwa nchini Kenya.

Mkuu wa wilaya la Longido ulipo mpaka huo, Frank Mwaisumbe, alisema wilaya hiyo imeimarisha ukaguzi katika mpaka wa Namanga.

Wafanyabiashara wanaozunguka mpaka huo wanaeleza kuwa biashara zao zimeyumba hasa baada ya Kenya kutangaza visa vya corona.

Sara Keiya, mfanyabiashara wa shanga na urembo katika mpaka huo, aliiambia DW kwmaba wateja wengi kwa sasa hawawasogelei wafanyabiashara na "wafanyabiashara wenyewe wanaogopa kuwasogelea wateja kwa hofu ya kupata maambukizi ya corona."


Veronica Natalis, DW Arusha