1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru: Waasi wa M23 waanza kuelekea Bukavu

29 Januari 2025

Wakati taarifa zikieleza kuwa waasi wa M23 wameanza kuelekea huko Bukavu, Rwanda imetahadharisha kuwa kundi hilo huenda likachukua udhibiti wa maeneo mengine zaidi huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4pnC8
Mji wa mashariki mwa Kongo wa Bukavu
Mji wa mashariki mwa Kongo wa BukavuPicha: GUERCHOM NDEBO/AFP

Kauli hiyo ya Rwanda imetolewa na Balozi wake katika eneo la Maziwa Makuu Vincent Karega aliyesema kwamba M23 wataendelea kusonga mbele zaidi ndani ya ardhi ya Kongo na kwamba Goma haiwezi kuwa lengo pekee la M23 isipokuwa kufanyike mazungumzo kati ya kundi hilo na serikali ya Kongo, jambo ambalo hata hivyo amesema analitia shaka.

Serikali mjini Kinshasa imedhihirisha mara kadhaa msimamo wake kuwa kamwe haitozungumza na M23  wanaoungwa mkono na Rwanda ambao sasa inawachukulia kama magaidi.

Baada ya kauli hiyo, vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa waasi hao wa M23 sasa wameanza kusonga mbele kuelekea Bukavu ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.

Wanajeshi wa DRC na mamluki wajisalimisha

Waasi wa M23 walipokuwa Keshero wakielekea katika mji wa Goma
Waasi wa M23 walipokuwa Keshero wakielekea katika mji wa GomaPicha: -STR/AFP

Hali bado ni tete huko Goma licha ya M23 kuutwaa kabisa mji huo. Mamia ya wanajeshi wa Kongo pamoja na mamluki kutoka Romania wamejisalimisha kwa jeshi la Rwanda, huku maelfu ya raia wa Kongo wakiyakimbia mapigano.

Ubelgiji imewataka raia wake kutosafiri kuelekea Kongo kutokana na sababu za kiusalama, siku moja baada ya waandamanaji kuzilenga balozi kadhaa mjini Kinshasa. Shirika la Brussels airlines limesitisha hivi leo safari zake zote kuelekea mjini Kinshasa.

Soma pia: Marekani yaitaka Rwanda kujiondoa katika mji wa Goma

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kukomesha ghasia zinazoendelea mashariki mwa Kongo.

"Ninaelezea wasiwasi wangu kuhusu hali mbaya ya usalama huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ninaziomba pande zote katika mzozo huu zichukue hatua za kusitisha mapigano na kuwalinda raia wa Goma na maeneo mengine yaliyoathiriwa na harakati za kijeshi. Wakati nikifanya maombi kwa ajili ya kurejeshwa haraka kwa amani na usalama, ninawataka viongozi wa eneo hilo na jumuiya ya kimataifa kufanya kila jitihada ili kusuluhisha mzozo huu kwa njia za amani."

Juhudi za kimataifa na kikanda zinaendelea

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi Picha: Boniface Muthoni/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Katika harakati za kuutafutia suluhu mzozo huo wa Mashariki mwa Kongo ambao umesababisha kutokea kwa hali mbaya zaidi ya kibinaadamu, juhudi mbalimbali za kimataifa na kikanda zinaendelea.

Leo usiku, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  Felix Tshisekedi anatarajiwa kulihutubia taifa hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo wa Mashariki mwa nchi yake.

Baadaye jioni ya siku ya Jumatano, kunatarajiwa pia mkutano wa jumuiya ya Afrika Mashariki uliotishwa na rais wa Kenya William Ruto na utakaofanyika kwa njia ya video, mkutano ambao Tshisekedi amesema hatohudhuria.

(Vyanzo: AFP, Reuters, DPA, APE)