1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru mpya ya mazungumzo Sudan, Je itamaliza mkwamo?

Sylvia Mwehozi
13 Mei 2019

Viongozi wa kijeshi wa Sudan na waandamanaji watafanya duru mpya ya mazungumzo kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, wakati waandamanaji wakiendelea kupiga kambi nje ya jeshi

https://p.dw.com/p/3IOpj
Sudan Pressekonferenz der Opposition
Picha: picture-alliance/AA/O. Erdem

Mnamo siku ya Jumamosi muungano wa uhuru na mabadiliko ambao ni mwamvuli wa vuguvugu la waandamanaji, ulisema viongozi wa kijeshi walituma mwaliko wa mazungumzo mapya baada ya siku kadhaa za mkwamo. Msemaji wa muungano huo Rashid al-Sayed alisema awali mazungumzo hayo yalikuwa yafanyike Jumamosi lakini yakaahirishwa hadi Jumatatu.

Sayed hakufafanua kwanini mazungummzo hayo yalisogezwa mbele, lakini vyanzo tofauti ndani ya muungano vinasema kulihitajika muda zaidi kwa ajili ya mashauriano zaidi ya kiutawala. Baadae siku ya Jumapili, msemaji wa baraza la kijeshi linalotawala Luteni Shamseddine Kabbash alithibitisha duru mpya ya mazungumzo. Kabbashi ameongeza kuwa mazungumzo yanafanyika katika "mazingira yenye kutia moyo" ili kufikia makubaliano ya kipindi cha mpito.

Afrika | Protests im Sudan
Waandamanaji wa Sudan wakiwa mtaaniPicha: picture-alliance/dpa/AA/M. Hjaj

"Tunakubaliana nao juu ya muundo wa jumla wa mfumo wa kiutawala wakati wa kipindi cha mpito kwa kuzingatia baraza huru, mfumo wa serikali, mfumo wa bunge na mifumo mingine. Tulichogundua ndani ya pendekezo lao lililowasilishwa kwetu ni kwamba waliondoa chanzo cha sheria. Maoni yetu ni kwamba Sharia ya Kiislamu na tamaduni katika Jamhuri ya Sudan viwe ndio chanzo cha sheria".

Duru hiyo mpya ya mazungumzo inakuja mnamo wakati maelfu ya waandamanaji wakisalia kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum. Wanasema wamedhamiria kulishinikiza Baraza la Kijeshi kukabidhi madaraka, kama ambavyo walivyomuondoa Omar al-Bashir.

Viongozi wa kijeshi na waandamanaji wanatofauatina juu ya nani ataliongoza Baraza la mpito. Jeshi linapendekeza Baraza jipya liongozwe kijeshi, huku waandamanaji wakitaka uwakilishi mkubwa wa raia ndani ya baraza hilo. Mwishoni mwa mwezi uliopita, muungano wa upinzani uliwasilisha mapendekezo yao kwa jeshi kuhusiana na serikali ya mpito itakayoongozwa kiraia.

Wakati huohuo waandamanaji wamezuia mtaa mkubwa unaopatikana kando ya mto Nile kwa kutumia mawe na miti, baada ya vikosi vya usalama kuwazuingia kuingia eneo ambalo wenzao wamepiga kambi. Baraza la kijeshi limelaani kitendo hicho likisema "hakikubaliki na kinachochea vurugu na kufanya maisha kuwa magumu kwa raia wengine".

AFP