1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha Siku ya Mazingira

Admin.WagnerD5 Juni 2015

Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yameng'oa nanga leo hii, huku wito ukitolewa na Umoja wa Mataifa kwa serikali, jamii na watu binafsi kuboresha mienendo yao ya matumizi ya raslimali.

https://p.dw.com/p/1Fc5t
Palästina Ban Ki-moon in Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon.Picha: picture-alliance/dpa/M. Saber

Shughuli za kuadhimisha siku ya mazingira Duniani zimeanza rasmi leo hii na mwaka huu kauli mbiu ni 'Ndoto bilioni saba. Sayari Moja. Tumia kwa kujali.'

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, lengo kwa mwaka huu ni kukuza suala la maendeleo endelevu, ili kuboresha hali ya maisha kwa wote duniani bila ya kuchochoe uharibifu wa mazingira, na bila ya kuhatarisha raslimali zinazohitajika kwa vizazi vijavyo.

" Kuanzia mwaka huu tujitahidi tuwe waangalizi bora wa dunia yetu," amesema Ban.

Ban aliongeza katika mwaka huu wa mabadiliko, kuna mategemeo ya kusonga mbele katika masuala ya maendeleo endelevu na mabadiliko ya tabia nchi. Amesisitiza siku ya leo iadhimishwe kwa kuwa waangalifu zaidi, juu ya athari zetu kama binaadamu juu ya viumbe na mazingira.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa mpango wa mazingira wa Umoja wa Mataifa, Achim Steiner, amesema katika maisha ya dunia hii ya utandawazi yenye watu bilioni 7, ni rahisi sana kupuuza athari za binaadamu juu ya mazingira.

Aliendelea kwa kusema kuwa maadhimisho haya ya kila mwaka, yanawakumbusha watu dunia nzima kuwa ni uwamuzi wetu sisi binadamu ambao unaijenga dunia.

"Maamuzi yetu na matumizi yetu ya kila siku ya mabilioni ya watu yana athari kwa mazingira. Baadhi ya matumizi ya kila siku yanachangia katika kupungua kwa maliasili, lakini baadhi pia ya vitendo vya binaadamu vinasaidia kuhifadhi mazingira. Sasa uwamuzi ni wetu sisi," amesema Steiner.

Jukumu la kila mmoja ya watu bilioni saba

Steiner amesema matumizi mabaya yasiyokuwa endelevu pamoja na uzalishaji wa viwanda, ni miongoni mwa sababu kubwa za uharibifu wa mazingira.

Hakuna shaka kuwa katika miaka 50 iliyopita tumeona mabadiliko makubwa ya mahusiano baina ya wanaadamu na mazingira yaliyomzunguka, hususan katika ongezeko la matumizi yasiyo endelevu ya maliasili, ambalo limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Steiner amesema angependa kila mmoja kufikiria dunia itakuwa wap,i ikiwa kila mmoja kati ya watu bilioni 7 atachangia katika kuleta mabadiliko ya matumizi bora ya raslimali yenye busara. Wito wake ni kwa kila mmoja kujitahidi kutekeleza hilo, hata kama ni kwa kukataa kutumia mifuko ya plastiki ama kupanda baiskeli badala ya gari ama basi kwenda kazini.

Mwandishi:Yusra Buwayhid/unep website

Mhariri:Josephat Charo