1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yajiandaa kutoa chanjo ya kwanza ya ugonjwa wa Ebola

Sylvia Mwehozi
21 Mei 2018

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inajiandaa kuzindua mpango wa chanjo ya kwanza leo Jumatatu, katika jitihada za kukabiliana na mripuko wa hivi karibuni wa ugonjwa hatari wa Ebola.

https://p.dw.com/p/2y3hv
Kongo Ebola Impfstoff in Kinshasa
Picha: Reuters/K. Katombe

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetaja idadi ya vifo vilivyotokana na ugonjwa huo kufikia 25, huku visa vitatu vipya katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi vikithibitishwa na waziri wa afya wa nchi hiyo katika kauli aliyoitoa siku ya jumamosi. Kitisho cha ugonjwa huo  ambao awali uliripotiwa maeneo ya vijijini yasiyofikika kwa urahisi, kilishika kasi wiki iliyopita, hasa baada ya kisa cha kwanza kuthibitishwa katika mji wa Mbandaka ulio na wakazi milioni 1.2

Serikali ya Congo imesema chanjo za kwanza zitawalenga wafanyakazi wa afya huko kaskazini magharibi ambao wamekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja au yasiyo moja kwa moja na wagonjwa. Miongoni mwao ni Daktari Hilaire Manzibe kutoka hospitali ya rufaa ya Wangata ambaye alimtibu mgonjwa mmoja mnamo Mei 1 aliyewasili kutokea Bikoro, kitovu cha mripuko wa sasa na aliyekuwa na dalili za homa na kutapika.

Kongo Ebola Behandlungszentrum in Bikoro
Mfanyakazi wa afya katika kituo cha afya cha BikoroPicha: picture-alliance/AP Photos/UNICEF/Mark Naftalin

Hata hivyo, familia ya mgonjwa huyo ilikataa kutibiwa na badala yake kumrejesha nyumbani ili apatiwe tiba za kienyeji, moja ya kizingiti kigumu ambacho kimekuwa kikwazo katika mripuko uliopita wa 2014. Wiki moja baadae mgonjwa huyo alirejea akionyesha dalili zote za homa iliyoukumba mji wa bikoro.

Mmoja wa wakazi wa mji wa Mbandaka, Jean Anthoine, anasema hajawahi kumuona mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo, akiwakilisha wakazi wengi wa mji huo walosema hawana elimu ya kutosha kujikinga na Ebola. "Binafsi sijawahi shuhudia mtu aliyefariki na Ebola. Tupo kwenye maboti yetu kila siku kwenye ziwa, tunaenda kwenye vijiji vya jirani kutafuta wateja, hatujui chochote kuhusu mripuko wa Ebola hapa Mbandaka."

Shirika la afya duniani WHO limesambaza wataalamu wa chanjo wapatao 35, wakiwemo 16 waliokusanywa wakati wa mripuko wa ugonjwa huo afrika magharibi ulioanza mwaka 2013. Timu iliyobaki ni wataalamu wapya kutoka Congo waliopatiwa mafunzo. Jumla ya chanjo 600 zinatarajiwa kutolewa. Wafadhili wameahidi dozi laki 3 za chanjo, kwa mujibu wa msemaji wa serikali, ambapo hadi sasa 5,400 tayari zimepokelewa.

Uganda Körpertemperaturmessung wegen Ebola-Ausbruch im Kongo
Uganda ikipima abiria uwanja wa ndege kutokana na mripuko wa ebola nchi ya DRCPicha: picture-alliance/dpa/XinHua/J. Kiggundu

Siku ya Jumamosi, Waziri wa Afya Oly Ilunga Kalenga alisema visa vitatu vipya vimeripotiwa mjini Mbandaka:

"Wikiendi hii kumeripotiwa visa vipya viwili vya homa katika kituo cha afya cha wangata, moja ya kituo cha afya katika mji wa Mbandaka. Baada ya uchambuzi, moja ya sampuli mbili zilithibitisha ugonjwa wa Ebola."

Mjini Geneva, WHO ilisema kati ya visa 45 vilivyorekodiwa, 14 kati yake vimethibitishwa na vipimo vya maabara. Lakini shirika hilo lilisema siku ya Ijumaa kwamba mripuko wa karibuni wa Ebola hauwezi kutajwa kama dharura ya kutia wasiwasi jumuiya ya kimataifa, na kuongeza kwamba mwitikio wa Kinshasa yenyewe umekuwa wa haraka na wa kina.

Serikali ilitangaza mripuko wa virusi hatari vya Ebola katika jimbo la kaskazini magharibi la Equateur mnamo Mei 8. Ebola ni ugonjwa hatari na wa kuambukiza ambao unafanya vigumu kukabiliana nao hususan katika maeneo ya vijijini ambako watu huingiliana zaidi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp

Mhariri: Mohammed Khelef