1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaizaba Augsburg na kukamata usukani wa ligi

22 Mei 2023

Borussia Dortmund inahitaji ushindi wa mechi moja tu katika siku ya mwisho wa msimu Jumamosi ijayo ili kuhitimisha utawala wa miaka 10 wa Bayern Munich kama mabingwa wa Bundesliga.

https://p.dw.com/p/4ReWD
Deutschland Bundesliga FC Augsburg - Borussia Dortmund | Sebastien Haller
Picha: Revierfoto/IMAGO

Hii ni kufuatia ushindi wa mabao matatu kwa sifuri jana Jumapili dhidi ya Augsburg. Sebastian Haller ambaye alikosa mzunguko wa kwanza wa msimu kutokana na matibabu ya saratani, alifunga mabao mawili ya kwanza kabla ya Julian Brandt kufunga la tatu katika muda wa nyongeza.

Dortmund ambao walikuwa mabingwa wa ligi mara ya mwisho mwaka wa 2012,  waliwaondoa Bayern kileleni mwa ligi kwa pengo la pointi mbili. Bayern walifungwa mabao matatu kwa moja na nambari tatu kwenye ligi RB Leipzig Jumamosi.

Dortmund itacheza dhidi ya Mainz katika dimba la nyumbani wakati Bayern watakuwa ugenini dhidi ya Köln. VfB Stuttgart iliondoka katika nafasi za kushushwa daraja baada ya ushindi wa 4 -1 dhidi ya Mainz.