1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

De Bruyne na Witsel kuikosa mechi ya ufunguzi ya Euro

11 Juni 2021

Kiungo wa timu ya taifa ya Ubelgiji Kevin De Bruyne ataikosa mechi ya ufunguzi ya timu yake dhidi ya Urusi katika michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2020.

https://p.dw.com/p/3ulnh
Portugal Porto | UEFA Champions League Finale | Kevin De Bruyne Verletzung
Picha: MICHAEL STEELE/AFP

Kiungo wa timu ya taifa ya Ubelgiji Kevin De Bruyne ataikosa mechi ya ufunguzi ya timu yake dhidi ya Urusi katika michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2020.

De Bruyne alipata jeraha la uso katika mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa mnamo Mei 29 dhidi ya Chelsea, wakati timu yake ilipofungwa 1-0, na alitakiwa kufanyiwa upasuaji.

Kupitia ukurusa wa Twitter, timu hiyo imeandika kuwa kiungo Axel Witsel pia ataikosa mechi hiyo ya ufunguzi.

Staa huyo wa Manchester City tayari alikuwa amedokeza kuwa huenda angeikosa mechi ya ufunguzi wakati wa mkutano na mfalme Philippe wa Ubelgiji.

"Je, nitaweza kucheza mechi ya ufunguzi? Natumai labda nitakuwa fiti katika mechi ya pili dhidi ya Denmark," alinukuliwa na vyombo vya habari vya Ubelgiji.

De Bruyne anatajwa kuwa mchezaji muhimu kwa timu hiyo ya taifa inayoorodeshwa nambari moja duniani, na kikosi chao kinachukuliwa kama "kizazi cha dhahabu" wakati kinaposaka ufalme wa soka barani Ulaya mwaka huu baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kombe la dunia la mwaka 2018.

Deutschland Bundesliga RB Leipzig - Borussia Dortmund | Axel Witsel
Kiungo wa Borussia Dortmund Axel WitselPicha: Ronny Hartman/REUTERS

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na chama cha wachezaji wa kulipwa nchini Uingereza kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuisadia Manchester City kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya Premia.

Uwepo wa kiungo wa Borussia Dortmund katika kikosi cha timu ya taifa kuliwashangaza wengi hasa ukizingatia kuwa kiungo huyo hajacheza mechi yoyote tangu mwezi Januari baada ya kupata jeraha.

Eden Hazard wa Real Madrid pia amekuwa akisumbuliwa na majeraha mbalimbali msimu huu japo anatarajiwa kuwa fiti wakati Ubelgiji itakapoingia uwanjani kesho Jumamosi 12.06.2021 kuvaana na Urusi.