1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dar Es Salaam. Mpango wa kupambana na ukimwi wazinduliwa.

21 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEsT

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton amezindua mpango mpya wa kupambana na ukimwi nchini Tanzania jana , akitoa wito wa kupambana kwa nguvu zote kuzuwia ueneaji wa ugonjwa huo mbaya na kurefusha maisha ya wale ambao tayari wameathirika.

Hadi pale ambapo tutaongeza kasi, nguvu na kupata mafanikio , juhudi za kupambana na ukimwi hazitapata mafanikio , Clinton amesema wakati yeye pamoja na rais wa Tanzania Benjamin Mkapa wakizindua mpango huo mpya ambao una lengo la kuimarisha matibabu katika maeneo ya vijijini katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Bwana Clinton amewasifu viongozi wa Tanzania kwa mpango wao unaoendelea wa kupambana na ukimwi , lakini amesema juhudi zaidi zinahitajika kuwahudumia watu zaidi ya milioni 2 ambao wameathirika na virusi vya ukimwi.

Kwa nchi yenye kipato cha chini kama Tanzania , hii ni changamoto kubwa na kuna safari ndefu, amesema Clinton , akielezea ukweli kwamba wengi wa wananchi wa Tanzania wanaofikia milioni 38 wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku.