1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Damascus. Waziri ajiua, kabla ya ripoti ya umoja wa mataifa.

12 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CESc

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Ghasi Kanaan amejiua. Taarifa hizo zinakuja siku chache kabla ya umoja wa mataifa kutoa matokeo ya uchunguzi juu ya kuuwawa kwa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri mapema mwaka huu.

Kanaan anaripotiwa kuwa alihojiwa mara kadhaa juu ya kifo cha Bwana Hariri. Kanaan aliwahi kuwa mkuu wa masuala ya ujasusi nchini Lebanon kutoka katika miaka ya 1980 hadi 2003.

Waziri huyo wa mambo ya ndani , alizungumza na radio moja ya Lebanon leo Jumatano kabla ya kujiua na kusema kuwa hilo litakuwa tamko lake la mwisho.

Katika taarifa yake hiyo katika radio inayojulikana kama Voice of Lebanon ametetea kuwepo kwa majeshi ya Syria nchini Lebanon, akisema kuwa majeshi ya nchi yake yamefanya kila kinachowezekana kuweza kuweka hali ya umoja nchini Lebanon.

Kanaan mwenye umri wa miaka 63 amesema taarifa za vyombo vya habari tangu Februari 14 alipouwawa Bwana Rafik Hariri zimekwenda kinyume na yeye binafsi pamoja na waziri mkuu huyo wa zamani, ambaye kuuwawa kwake kwa kiasi kikubwa kumehusishwa na Syria licha ya kukana kwa mara kadha.