1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAILY NEWS LAPIGWA MARUFUKU-ZIMBABWE

17 Septemba 2003
https://p.dw.com/p/CHeQ

Uhuru wa vyombo vya habari vimepata pigo kubwa nchini Zimbabwe,baada ya gazeti huru pekee kulazimishwa kufungwa na kunyanganywa zana zake. Gazeti la Daily News lilifungwa Septemba 12,baada ya gazeti hilo kushindwa kesi katika Mahakama Makuu.Daily News limepinga sheria inayovitaka vyombo vya habari na waandishi habari kujiandikisha katika shirika lilichoaguliwa na serikali.Siku nne baada ya kushindwa kesi hiyo,polisi walizisaka ofisi za Daily News na kunyanganya kompyuta na vyombo vingine vya uchapishaji,alieleza mwanasheria wa Daily News Gugulethu Moyo.Hali ya wasi wasi ilianza kuzuka baada ya Mahakama Makuu kupitisha uamuzi wake na gazeti la Daily News kutoonekana mitaani Septemba 12.Wakati huo huo ripoti zilisema kuwa wakuu wa gazeti hilo wanakabiliwa na mashtaka kuwa walifanya kazi kinyume na sheria kwani gazeti hilo halijasajiliwa kama sheria inavyotaka-sheria ambayo hupingwa na Jumuiya ya Magazeti nchini Zimbabwe ANZ kampuni inayochapisha gazeti la Daily News.Sheria hiyo inatazamwa kama ni sehemu ya silaha ya serikali ya Zimbabwe kudhibiti vyombo huru vya habari vilivyo vichache,lakini hupaza sauti.

Sheria hiyo iliyopitishwa March mwaka 2002 inakosolewa kwa sababu imeweka vizingiti kwa wale wanaotaka habari kutoka mashirika ya kiserikali.Vile vile kuambatana na sheria hiyo kumeundwa Tume ya Habari na Vyombo vya Habari inayodhibitiwa na serikali ambako kila mwaandishi habari na vyombo vyote vya habari vile vile vinapaswa kuandikishwa.

ANZ imepinga masharti mengi kuhusu usajili,hasa sharti la kutoa maelezo ya kibinafsi kuhusu wakurugenzi wake na uhusiano wao wa kisiasa,mipango ya biashara na ya pesa kwa miaka miaka mitano ijayo.Yasemekana kuwa kampuni ya ANZ haipo pekee katika upinzani wake.Hata Jumuiya ya waandishi huru wa habari nchini Zimbabwe IJAZ-inapinga vifungu fulani vya sheria hiyo na inangojea uamuzi wa kesi yake katika Mahakama Makuu.

Licha ya hayo yote,kampuni ya ANZ imesema ipo tayari kujiandikisha mapema iwezekanavyo,lakini mkuu wa Tume ya Habari na Vyombo vya Habari Bwana Tafataona Mahoso amesema utaratibu wa kusajili huenda ukachukua muda.

Hatua ya kulifunga gazeti la Daily News limelaaniwa sehemu mbali mbali nchini Zimbabwe.Tawi la Zimbabwe la Taasi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika,limesema kufungwa kwa ghafla gazeti la Daily News,kumeinyanganya nchi uwezekano mdogo uliokuwepo kwa wananchi kujieleza kwa uhuru katika hali ambayo inazidi kubanwa.Kwa maoni ya mchambuzi wa kisiasa John Makumbe sasa wasomaji wa magazeti watajua kile tu ambacho chama tawala ZANU-PF kinawataka wajue.Kawaida wajibu wa mahakama ni kushughulika na mizozo kati ya wananchi,lakini safari hii mahakama inasema sheria isiyo na haki ifuatwe,aliongezea Makumbe.Kwa upande mwingine Paul Themba Nyathi wa chama cha upinzani MDC amesema,hili ni pigo la mpito tu kwani wananchi wa Zimbabwe watalirejesha gazeti mitaani kama inavyostahilika.