1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wasema Afrika Magharibi kukabiliwa na njaa

Ibrahim Swaibu
28 Mei 2020

Vizuizi viliowekwa na serikali za Afrika Magharibi kupambana na COVID-19 vimeyumbisha biashara ya bidhaa zinazoharibika kwa haraka  pamoja na biashara ya mifugo.

https://p.dw.com/p/3csyP
Hunger im Sahel Bildergalerie Tschad
Picha: Andy Hall/Oxfam

Katika nyakati za kawaida kabla ya janga la virusi vya Corona, Boureima Diawara anayefanya biashara ya kuuza maembe anasema, alikuwa akichukua siku tatu  kusafirisha bidhaa hizo  kutoka kusini mwa nchi ya Mali hadi Dakar, mji mkuu wa Senegal, safari yenye umbali wa kilomita 1,200.

Lakini tangu kuwekwa kwa  vizuizi vya kudhibiti virusi vya Corona katika nchi za Afrika Magharibi, Diawara anaeleza kuwa, sasa anachukua zaidi ya siku 6. Isitoshe, baada ya kuchelewesha katika mipaka pamoja na zuio la kutembea usiku nchini Senegal, wafanyakazi wake wanalazimika  kutupa magunia ya maembe yaliooza majalalani.

Vizuizi viliowekwa na serikali za Afrika Magharibi kupambana na COVID-19 vimeyumbisha biashara ya bidhaa zinazoharibika kwa haraka  pamoja na biashara ya mifugo.

Umoja wa mataifa umeonya kuwa kukwamisha kwa biashara kunaongeza wasiwasi  wa kutokea kwa uhaba wa chakula katika eneo la Afrika Magharibi. Shirika hilo la kimataifa linasema janga la COVID-19 huenda likasababisha kuongezeka mara mbili kwa idadi ya wakaazi wa Afrika Magharibi wenye ukosefu wa chakula kufikia watu milioni 43 katika kipindi cha miezi sita zijazo.

Kwa mujibu wa data za Kamati ya Kudumu ya Kudhibiti ueneaji wa jangwa katika eneo la Sahel, wafanyabiashara wa bidhaa zinazoharibika kwa haraka wamepata khasara ya asilimia 10.

Kadhalika data hizo zimeonyesha kuwa wale wanaojishughulisha na biashara ya mifugo wamekabiliwa na asilimia 30 ya khasara katika biashara yao.

Shughuli zakwamishwa

Wakati huo huo, utafiti wa wafanyabiashara wa mifugo, Afrika Magharibi umebaini kuwa kwa sasa asilimia 42 ya shuguhuli za kiuchumi kwa wafugaji zimesitishwa.

Mnamo Machi, Mauritania ilifunga mpaka wake na Senegal ambayo ndio soko kuu la mifugo yake. Hata kama mizigo na bidhaa mbalimbali inaruhusiwa kupita. Lakini kwa upande wa wafugaji,  wizara ya kilimo ya Mauritania inasema inashikilia msimamo wake wa kutowaruhusu wafugaji ha mifugo yao hadi nchini Senegal 

Kenia Rinderhüter und Rinder in Kajiado
Picha: dapd

Nako nchini Benin, wafanyabiashara walikuwa tayari wanakabiliwa na changamoto hata kabla ya vizuizi vya kudhibiti Corona kuwekwa.

Hii ni kufuatia Nigeria kufunga mpaka wake na nchi hiyo mnamo Agosti mwaka uliopita kutokana na kile serikali ya rais Muhammadu Buhari ilisema ni kukabilana na magendo katika mpaka huo.

Hatahivyo, katika wiki za hivi karibuni, baadhi ya serikali zimeanza kulegeza vizuizi  kama mojawapo ya hatua kuzuia kuporomoka kwa uchumi ikiwemo kufungua masoko na kupunguza muda wa marufuku ya kutembea.

Mkrugenzi mkuu wa kilimo, fedha na maendeleo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, Atsuko Toda amezisifu serikali hizo kwa kupunguza vizuwizi vya usafirishaji wa chakula kutoka mataifa yao hadi ya Kigeni. Mtaalmu huyo ameeleza kuwa hatua hiyo ni ishara ambayo itaweza kuzuia kupanda kwa bei ya chakula na hivyobasi kuziuia janga lingine la uhaba wa chakula kama ambavyo ilitokea mnamo mwaka 2007-2008.

Katika eneo la Afrika Magharibi, biashara ya chakula, kwa kiasi kikubwa huendeshwa na wafanyabiashara wenye biashara ndogo ndogo ambao huuza bidhaa ikiwemo  kuku, vitungu,  ndizi nakadhalika. Wafanyabiashara hao  hutumia usafiri wa umma kusafirisha mifugo kutoka nchi moja hadi nyingine.

Chanzo: Reuters