1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo itakuwa mwanachama rasmi wa EAC

22 Desemba 2021

Mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki umeridhia ombi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kujiunga na jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/44iUh
Treffen von Führungspersönlichkeiten der Ostafrikanischen Gemeinschaft
Picha: Arusha Veronica Natalis/DW

Hii ni baada ya kujiridhisha na faida za moja kwa moja za ushirikiano na taifa hilo kubwa kieneo kusini mwa jangwa la sahara. Mkutano huo umefanyika  kwa njia ya mtandao  na kuhudhuriwa pia na viongozi wengine wa jumuiya hiyo katika makao yake makuu yaliyopo Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Ni katika ukumbi huu mkubwa wa mikutano uliopo hapa katika ofisi za makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha Tanzania, viongozi mbali mbali wa jumuiya hiyo  wanafuatilia moja kwa moja mmkutano huu wa  18 wa wakuu wa nchi  sita kupitia luninga. 

soma Baraza la Biashara Afrika Mashariki laingilia mzozo Kenya, Uganda

Mwenyekiti wa wakuu hao wa nchi ambaye ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyata wakati akifungua mkutano huo alibainisha kuwa mkutano umebebwa na ajenda kuu ya wakuu ya nchi kuridhia ombi la Congo kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki. Marais wote kwa kauli ya pamoja wamesema baada ya kukamilika kwa hatua zilizosalia Congo itakuwa rasmi mwanachama wa jumuiya hiyo, kama anavyoeleza Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

soma Biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki imeshuka

"Kuhusu Congo kuwa mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, tunatazamia kuona hatua zilizosalia zinakamilika na tuafurahi kuwa nao kwenye jumuiya yetu.” alisema Kagame.

Siku muhimu kwa jumuiya ya Afrika Mashariki

Treffen von Führungspersönlichkeiten der Ostafrikanischen Gemeinschaft
Picha: Arusha Veronica Natalis/DW

Rais wa Tanzania Samia Suluhu amesema "Waheshimiwa leo ni siku muhimu sana, ni siku ya kutengeneza historia mpya kwa jumuiya yetu. Tumepitia ripoti ya mawaziri tumeipitisha na tunatazamia kukamilika kwa hatua zingine za mbele ili Congo iwe mwanachama kamili.”

Kulingana na jumuiya ya Afrika mashariki kufikia mwezi Machi mwaka Kesho 2022 hatua zote zitakuwa zimekamilika na Congo itakuwa tayari ni mwanachama wa jumuiya hiyo. 

Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo iliyo na idadi ya watu wanaofikia milioni 90 na inayopakana na nchi tano za jumuiya, iliomba kujiunga na taasisi hiyo ya kikanda mnamo mwezi Februari mwaka huu 2021, na kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo , nchi nyingine inaweza kujiunga  iwapo itaungwa mkono na nchi wanachama na iwapo nchi hiyo inayoomba itakuwa imetimiza masharti  ya uongozi bora, Demokrasia, utawala sheria, inayosheshimu haki za binadamu, na kwamba iwe jirani na mojawapo ya nchi  wanachama.

 

 

/Veronica Natalis DW Arusha.