1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chinamhora, Zimbabwe. Zimbabwe kufanya uchaguzi siku ya Alhamis.

29 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFSH

Wakati Zimbabwe itakapofanya uchaguzi wake mkuu wa bunge siku ya Alhamis suala litakalojitokeza kwa kiasi kikubwa katika mawazo ya wapiga kura ni hali mbaya ya kiuchumi katika nchi hiyo ambayo ilikuwa na hali bora kabisa.

Wakosoaji wa Bwana Mugabe wanasema kuwa licha ya kwamba eneo la mashambani ni nguzo kuu ya wapigakura wa rais huyo wa sasa, lakini raia hao wa mashambani wamekumbana sana na matatizo ya nchi hiyo ya kiuchumi na kisiasa.

Hali ya kukata tamaa imetanda katika baadhi ya maeneo ya vijijini na ni wakaazi wachache wanaoamini kuwa uchaguzi huo wa keshokutwa Marchi 31, ambapo chama cha Bwana Mugabe ZANU PF kinapambana na upinzani mkubwa kutoka chama cha Movement for Democratic Change, MDC, utaleta mabadiliko muhimu ya manufaa.

Wakati huo huo zaidi ya Wazimbabwe 1,000 walishiriki katika uchaguzi wa kuiga uliofanyika katika mji mkuu wa Afrika kusini Johannesburg leo, siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, wakipinga kunyimwa haki ya kufanya hivyo na serikali yao.

Nao wachapishaji wa gazeti la kila siku lililopigwa marufuku nchini humo la Daily News, wamesema kuwa gazeti hilo linaweza kuwafikia wasomaji katikati ya mwezi wa May kufuatia uamuzi wa mahakama wa kuondoa hatua hiyo ya serikali ya kulipiga marufuku gazeti hilo.