1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yazitahadharisha nchi za Magharibi dhidi ya kuitenga

18 Oktoba 2023

Mkutano kuhusu mradi wa kimataifa wa China wa miundo mbinu wahudhuriwa na wajumbe kutoka zaidi ya nchi 130

https://p.dw.com/p/4XgLs
China | Seidenstraßengipfel
Picha: Suo Takekuma/REUTERS

Rais Xi Jinping ameonya dhidi ya China kutengwa kiuchumi akizikosoa juhudi za nchi za Magharibi za  kupunguza kuutegemea uchumi wa taifa hilo.

Kiongozi huyo wa China ametoa onyo hilo wakati akifungua mjini Beijing mkutano kuhusu mradi mkubwa wa kimataifa  wa nchi yake wa  miundo mbinu ya reli na barabara.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi Jinping akifungua mkutano kuhusu mradi wa miundo mbinu ya barabara na reli(BRF)Picha: Edgar Su /REUTERS

Kongamano hilo limehudhuriwa na wajumbe kutoka zaidi ya nchi 130 wakiwemo viongozi wa juu wa serikali ambao ni pamoja na rafiki mkubwa wa rais Xi Jinping, Kiongozi wa Urusi Vladmir Putin.

Hii leo Jumatano akilifungua Kongamano hilo,Xi Jinping pamoja na kuzikosoa nchi za magharibi kwa kuendesha juhudi za kutaka mataifa yajiepusha kuutegemea uchumi wa nchi yake,ameusifu mradi wake huo mkubwa ulioanzishwa miaka 10 iliyopita wa kujenga miundo mbinu duniani pamoja na mifumo ya nishati inayoliunganisha bara la Asia na Afrika mpaka Ulaya kupitia baharini na nchi kavu,akisema ni mpango uliogeuka kuwa miradi halisi.

"Mivutano ya kiitikadi,uhasama wa siasa za kikanda na siasa za kimaeneo  sio jambo tunalolipendelea. Tunachokipinga ni vikwazo vinavyowekwa na upande mmoja,kubanwa na kutengwa kiuchumi pamoja na kuvurugwa kwa mifumo  ya usambazaji''

Reli inayounganisha  Budapest na Belgrad
Ujenzi wa reli kutoka Budapest, Hungary kwenda Belgrade, Serbia unaofadhiliwa chini ya mradi wa China wa BRIPicha: Attila Volgyi/Xinhua/dpa/picture alliance

Kiongozi huyo wa China amekwenda mbali zaidi katika kuzikosoa nchi za Magharibi akisema maisha hayawezi kuwa bora na wala maendeleo ya mataifa  hayawezi kuwa na kasi ikiwa yatajikita kutazama wengine kama kitisho na kuiona hatua ya kutegemea uchumi wa mwingine kama kitisho.

Rais huyo pia  ameyaahidi makampuni ya kigeni nafasi kubwa ya kufikia soko pana la China na ufadhili mpya wa zaidi ya dola bilioni 100 kwaajili ya kuyainua  mataifa yanayoendelea.

Hatua ya China kutowa vitisho dhidi ya kisiwa cha Taiwan pamoja na kuvurugika kwa biashara katika kipindi cha janga la Corona ni mambo yaliyoongeza mwamko wa dharura wa nchi za magharibi kutaka kupunguza kuitegemea China.

Japokuwa mradi wa miundo mbinu wa China mwanzoni uliorodhesha mpango wa kutaka pia kuiunganisha China na nchi za Ulaya Magharibi,mkutano huu unaofanyika Beijing haukuhudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Umoja wa Ulaya.

Kiongozi pekee wa serikali aliyekwenda kushiriki mkutano huo kutoka jumuiya hiyo ni waziri mkuu wa Hungary Victor Orban.

Rais wa kenya William Ruto
Rais wa kenya William RutoPicha: Jin Liwang)/Xinhua News Agency/picture alliance

Rais wa Kenya William Ruto ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioko kwenye kongamano hilo amesifu ushirikiano wa nchi yake na China akisema Kenya haina mashaka katika kukaribisha uwekezaji wa China.

Ama kwa upande mwingine  rais Vladmir Putin wa Urusi alioneshwa katika kanda ya video akiwa ameandamana na maafisa wake kwenye mkutano huo huku akiwa na kile kilichotambuliwa kuwa ni mkoba wenye taarifa za zana za Nuklia ,ambao kimsingi ndio unaotumiwa kuamrisha shambulio la Nuklia.Kanda hiyo ya video imechapishwa leo na shirika la habari la serikali.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW