1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaonya mataifa juu ya kitisho cha Vita Baridi vipya

6 Septemba 2023

Waziri mkuu wa China Li Qiang amesema kwamba mataifa makubwa yanalazimika kupinga makabiliano na Vita Baridi vipya na kusema upo uwezekano wa kukosekana makubaliano na mizozo kutokana na mitazamo tofauti.

https://p.dw.com/p/4W0BO
Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ASEAN-mjini Jakarta
Waziri mkuu wa China Li QiangPicha: Yasuyoshi Chiba/REUTERS

Waziri mkuu wa China Li Qiang amesema hii leo kwamba mataifa makubwa yanalazimika kupinga makabiliano na Vita Baridi vipya.

Qiang amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN huko Jakarta Indonesia na kusema upo uwezekano wa kukosekana makubaliano na mizozo kutokana na mitazamo tofauti, migongano ya kimaslahi na uingiliaji wa nje.

"Ili kuweza kuzidhibiti tofauti zetu, suala muhimu ni kuhakikisha tunapinga makabiliano ya kikanda na kupinga Vita Baridi vipya. Tofauti na mivutano baina ya mataifa ni lazima vyote vishughulikiwe ipasavyo," alisema Qiang. 

Qiang ametoa matamshi hayo wakati viongozi na maafisa wa ngazi za juu ambao ni pamoja na makamu wa rais wa Marekani Kama Harris wakitarajia kujadiliana masuala kadhaa yaliyogubika mikutano ya ASEAN wiki hii, ambayo ni pamoja na ramani ya China inayoonyesha umiliki wake wa eneo kubwa la Bahari ya China Kusini.