1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaonya kuhusu ongezeko la mzozo wa Ukraine

Saleh Mwanamilongo
21 Februari 2023

China inaelezea wasiwasi wake kwamba mzozo wa Ukraine unaweza kuwa mbaya zaidi kiasi cha kutoweza kudhibitiwa.

https://p.dw.com/p/4NmYQ
Indonesien Bali G20-Gipfel | Treffen Xi Jinping, Präsident China & Joe Biden, Präsident USA
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Beijing ambayo mwaka jana ilipiga jeki ushirikiano wake usio na kikomo na Moscow, imejiepusha kulaani uvamizi wa Urusi dhidi Ukraine. Marekani imeonya kuhusu madhara iwapo China itatoa msaada wa kijeshi kwa Urusi madai ambayo Beijing inakanusha.

Katika kongamano lililofanyika kwenye wizara ya mambo ya nje jijini Beijing, Qin Gang amesema China ina wasiwasi mkubwa kwamba mzozo wa Ukraine unaweza kuendelea kuongezeka au hata kutoweza kudhibitiwa.

"Wakati huo huo, tunazitaka nchi zinazohusika ziache kuongeza mafuta kwenye moto haraka iwezekanavyo, kuacha kuelekeza lawama kwa China, na kuacha kufanya fujo kwa kupiga kelele 'Leo Ukraine, kesho Taiwan'.", alisema Qin.

Maoni ya Qin yamefuatia taarifa za shirika la habari la Urusi TASS kwamba mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi alitarajiwa kuwasili Moscow Jumanne na kabla ya hotuba ya amani ya anayotarajiwa kutoa Rais Xi Jinping siku ya Ijumaa, ikiwa ni maadhimisho ya mwaka mmoja wa uvamizi wa Ukraine.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema ziara ya Wang nchini Urusi itakuwa fursa ya kukuza zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Je, China inaipatia Urusi silaha?

China bado mshirika muhimu zaidi wa biashara wa Urusi
China bado mshirika muhimu zaidi wa biashara wa UrusiPicha: CHRISTOF STACHE/AFP

Leo Jumanne, China ilitangaza mapendekezo yake kwa ajili ya mpango wa jumla wa usalama. Na pendekezo kuu la usalama la rais Xi linalenga kuzingatia kanuni ya "usalama usiogawanyika", pendekezo ambalo linaungwa mkono na Moscow.

Urusi imesisitiza kuwa serikali za Magharibi ziheshimu makubaliano ya mwaka wa 1999 kwa kuzingatia kanuni ya "usalama usiogawanyika", kwamba hakuna nchi inayoweza kuimarisha usalama wake kwa gharama ya wengine. Wakati wa zaira yake nchini Hungary hapo jana, Wang Yi alitoa wito wa kusuluhishwa kwa vita vya Ukraine kupitia mazungumzo.

Tofauti baina ya China na Marekani

Marekani inazitaja China na Urusi kama nchi mbili ambazo ni tishio kubwa kwa usalama wake. Jumamosi Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliionya China kuwa msaada wa silaha kwa Urusi utaathiri uhusiano baina ya China na Marekani. Kwa upande wake Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell, aliionya China kwamba kuipatia Urusi silaha itakuwa imevuka mpaka.

Beijing imeishutumu mara kwa mara Washington kwa kuzidisha hali hiyo ya mgogoro kwa kuipatia Ukraine silaha.