1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

China yajitosa safari za sayari ya Mars

Josephat Charo
23 Julai 2020

Safari ya China kuelekea sayari ya Mars imeanza Alhamisi (23.07.2020) kama sehemu ya mpango wenye malengo makubwa ambao unatarajiwa kuendelea kwa miongo kadhaa ijayo.

https://p.dw.com/p/3fpdJ
China Marsmission Tianwen-1
Picha: Reutersw/C.G. Rawlins

China imezindua chombo cha anga za juu cha Tianwen-1 kuelekea katika sayari ya Mars, ikiwa ni ziara ya kwanza na yenye hatari ambapo taifa hilo linatarajia kupata nafasi kama taifa linalofanya utafiti katika anga za juu na kuingia katika kundi sawa na Marekani na Urusi.

Tianwen-1, ambayo maana yake ni "Maswali kwa Mbingu" ni chombo kinacholenga kufanya utafiti katika mazingira ya sayari ya Mars na kutafuta uwezekano wa dalili za uhai au maisha.

Roketi chapa Long March 5 lililokibeba chombo hicho limefyetuliwa kutoka kituo cha kufyetulia vyombo vya anga za juu cha Wenchang katika mkoa wa Hainan kusini mwa China saa sita na dakika 41.

Chombo hicho kitasafiri kwa takriban miezi saba kabla kufika Mars. Kitaizunguka sayari hiyo nyekundu kwa miezi miwili au mitatu kabla kujaribu kutua. Hapo ndipo sehemu ngumu ya safari hiyo itakapoanza - na China itakuwa nchi pekee inayojaribu kufanya hivyo.

Jumuiya ya Falme za Kiarabu ilizindua chombo chake kuelekea sayari ya Mars Jumapili iliyopita, huku kituo ha anga za juu cha Marekani, NASA, kikijiandaa kutuma chombo chake cha Perseverance rover wiki ijayo.

Vyombo vyote vitatu vya anga za juu vinatarajiwa kufika Mars Februari 2021.

Sababu kwa nini nchi zote tatu zinazindua safari hizo wakati mmoja ni kwamba sayari ya dunia na Mars hujongeleana karibu kila baada ya miezi 26, na hivyo kutoa mwanya wa fursa ya safari zisizotumia nishati nyingi na pia kutunishiana misuli katika anga za juu.

"Nadhani China inaweza kufanya hivi kama taifa lolote lengine, lakini sayari ya Mars ni changamoto," alisema mtaalamu wa masuala ya anga za juu wa Australia, Morris Jones.

China Raketen-Start Tianwen-1-Mission zum Mars
Roketi lililokibeba chombo cha Tianwen-1 likifyetuliwa kuanza safari kwenda MarsPicha: Getty Images/AFP

Awali safari za kwenda Mars zimekuwa na kasi ya ufanisi wa asilimia takriban 50, hata wakati zinapofanywa na nchi zenye uzoefu mkubwa zaidi katika kufanya utafiti katika anga za juu.

Hivi karibuni, chombo cha anga za juu cha Ulaya, Space Agency lander, kilianguka katika sayari ya Mars mwaka 2016, ingawa chombo cha Marekani kilifanikiwa kutua salama miaka miwili iliyopita.

"Kutua Mars ni kama kwenda jumba la kamari na kutia dau rangi nyekundu au nyeusi" alisema mtaalamu wa masuala a anga wa Ujerumani, Norbert Frischauf. "Fursa sio nzuri," aliongezea.

Mars ina nguvu kubwa zaidi inayovuta vitu chini kuliko mwezi na ina anga nyembamba, hali ambayo inaifanya kuwa vigumu kufunga breki wakati wa kutua.

Iwapo chombo cha Tianwen-1 kitafaulu, China itakuwa nchi ya tatu tu kupeleka chombo katika sayari ya Mars, baada ya Marekani na muungano wa zamani wa Sovieti.

China imetanua mpango wake wa safari za anga za juu katika miaka ya hivi karibuni na imepanga kufanya safari zaidi miongo kadhaa ijayo. Mwaka jana China ilikuwa nchi ya kwanza kupeleka chombo mwezini.

Mipango ya taifa hilo ni kujenga kituo cha anga za juu kufikia mwaka 2022 na kutuma chombo katika sayari ya Jupiter kufikia mwaka 2029.

(dpa)