1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yaanza luteka kubwa la kijeshi karibu na Taiwan

4 Agosti 2022

Siku moja baada ya Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, kumaliza ziara yenye utata kisiwani Taiwan, China, ambayo ilikasirishwa sana na ziara hiyo, inaanza mazoezi makubwa kabisa ya kijeshi kuzunguka kisiwa hicho.

https://p.dw.com/p/4F5sL
 Sea Guardians-2
Picha: Wang Guixian/Xinhua/picture alliance

Chama tawala nchini Taiwan kimesema kwamba mazoezi ya kijeshi ya China yanayoanza leo yamezusha mivutano ya kikanda na ni kinyume na sheria. 

Chama hicho, DPP, kimesema hatua ya China kufanya mazoezi ya kijeshi katika ujia wa bahari na eneo la anga kimataifa ni jambo linapuuzia wajibu wa kisheria na tabia ya kuchukuwa hatua za upande mmoja. 

China ilitangaza kwamba mazoezi makubwa ya kijeshi yanaanza kufanyika kwenye maeneo maalum sita yanayozunguka Taiwan hivi leo kufuatia ziara ya Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, iliyomalizika jana. 

China iliyopingana vikali na ziara hiyo iliyosema ni uchokozi wa wazi dhidi yake, iliapa kuchukuwa hatua kali na za haraka. 

Mazoezi hayo ya kijeshi yamepangwa kuanza saa 6:00 mchana kwa majira ya eneo hilo, na kwa mujibu wa vyombo vya habari vya China, yanafanyika umbali wa kilomita 20 tu kutoka fukwe za Taiwan na yatamalizika mchana wa Jumapili. 

Gazeti la serikali la Global Times limevinukuu vyanzo ya kijeshi limesema mazoezi hayo yatakuwa ya aina yake na kwamba makombora yatarushwa juu ya anga ya Taiwan kwa mara ya kwanza. 

Jibu kwa ziara ya Pelosi

Taiwan Nancy Pelosi, während eines Treffens mit der taiwanesischen Präsidentin Tsai Ing-wen
Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi (kushoto), akizungumza mbele ya Rais Tasi Ing-wen wa Taiwan mjini Taipei.Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Mazoezi yaliyoanza tangu siku ya Jumanne wakati Pelosi alipowasili Taiwan licha ya upinzani mkali wa China, yameweka mazingira ya kufanyika haya ya leo, ambayo shirika la habari la Xinhua limesema yataizingira Taiwan nzima.

Ofisi ya Bahari na Bandari ya Taiwan imetowa wito kwa meli kuepuka kupita maeneo ambayo China inafanya mazoezi yake ya kijeshi, ambayo baraza la mawaziri yanasema yanaingilia njia 18 za kimataifa za meli. 

China imetetea operesheni yake hii ya kijeshi ikisema ni ya lazima na ya haki, ikitupa lawama kwa Marekani na washirika wake katika ukanda huo.

"Kwenye mapambano ya sasa kutokana na ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan, Marekani ndiye mchokozi, China na muhanga," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China, Hua Chunying.

ASEAN yataka mvutano upozwe

 Sea Guardians-2
Mazoezi ya kijeshi ya China na Pakistan ya mwezi Julai 2022.Picha: Geng Haipeng/Xinhua/picture alliance

Hayo yakijiri, mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya ushirkiano wa kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, wamezitolea wito pande zote kujizuwia na kuifanya hali kuwa mbaya zaidi, wakionya kwamba inaweza kupelekea makabiliano ya moja kwa moja na mzozo wa wazi kati ya mataifa makubwa.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ambaye yuko mjini Phnom Penh kwa mazungumzo na wenzake wa ASEAN, ameikosowa hatua hiyo ya China, akisema hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha mazoezi ya kijeshi ya China yanayotishia uhuru na usalama wa Taiwan.