1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazima moto bado wanauizima moto katika mkasa wa Tianjin

14 Agosti 2015

Serikali ya China imesema itaanzisha ukaguzi kote nchini humo wa kusaka kemikali hatari na viripuzi baada ya miripuko miwili mikubwa iliyotokea katika mji wa bandarini wa Tianjin jana na kuwaua kiasi ya watu hamsini.

https://p.dw.com/p/1GFQ0
Picha: picture-alliance/Photoshot/Shen Bohan

Serikali ya China hii leo imesema imejifunza pakubwa kutokana na miripuko hiyo miwili mikubwa katika mabohari ya kuhifadhia kemikali na mitungi ya gesi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Baraza la mawaziri la China ambalo ndilo pia baraza la usalama limesema litafanya msako dhidi ya shughuli zisizo halali za kiviwanda ili kuhakikisha wanaimarisha usalama viwandani.

Shughuli za kuzima moto bado zinaendelea

Maafisa wa kikosi cha wazima moto takriban 1,000 hii leo wameendelea kujaribu kuuzima moto uliosababishwa na miripuko hiyo na kutambua kemikali hatari katika eneo la mkasa, siku mbili baada ya miripuko hiyo mikubwa ambayo wakaazi wa Tianjin wanahofu itawaathiri kiafya.

Afisa wa Uokozi katika kreni katika eneo la mkasa wa Tianjin
Afisa wa Uokozi katika kreni katika eneo la mkasa wa TianjinPicha: Reuters/D. Sagolj

Maafisa wa mji huo wa bandarini wenye shughuli nyingi za kiviwanda wamesema hawajajua mpaka sasa ni kemikali zipi hasa zilikuwa katika mabohari hayo yaliyoripuka au kiini cha miripuko hiyo.

Hata hivyo vyombo vya habari vya China na shirika la wanaharakati wa kuhifadhi mazingira la Greenpeace wameonya huenda kemikali zilizokuwa zimehifadhiwa zilikuwa hatari mno.

Greenepeace imeonya kuwa mvua huenda ikasafirisha kemikali hadi katika mabomba ya kupitishia maji na kuutaka utawala wa eneo hilo kufutailia kwa makini kisa hicho na kung'amua haraka iwezekanavyo ni aina gani ya kemikali zilikuwepo katika mabohari hayo.

Maafisa wa China kwa upande wao wametoa taarifa za kukinzana kuhusu uwezekano wa iwapo kemikali zilizokuwepo katika mabohari hayo ni ya viwango hatari mno kwa binadamu au la.

Kiasi cha watu 700 walijeruhiwa katika mkasa huo sabini kati yao vibaya sana. Miongoni mwa watu hamsini waliouawa katika mkasa huo ni wazima moto 17 na watu kadhaa hawajulikali waliko.

Afisa mmoja wa kikosi cha wazima moto hii leo ameokolewa kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka katika maksa huo. Zhou Ti mwenye umri wa miaka 19 amepelekwa hospitalini kutibiwa kwa maumivu ya kifua lakini hali yake inasemekana kuwa si mbaya.

Wataalamu kufanya uchunguzi kubaini chanzo

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya China la Xinhua limesema kundi la wataalamu 217 wa kinyuklia na kemikali za kibayolojia kutoka jeshi la nchi hiyo wamesafiri kuelekea Tianjin kufanya ukaguzi katika eneo la mkasa.

Maafa baada ya miripuko katika eneo la viwandani Tianjin China
Maafa baada ya miripuko katika eneo la viwandani Tianjin ChinaPicha: Reuters/China Daily

Kuambatana na sheria za China, mabohari ya kuhifadhia kemikali na bidhaa nyingine hatari kwa usalama wa binadamu yanapaswa kuwa umbali wa angalau kilomita moja kutoka maeneo ya makaazi, majengo ya umma na barabara kuu.

Katika kisa cha Tianjin, nyumba mbili za makaazi na barabara kuu kadhaa zilikuwa karibu na mabohari hayo. Hospitali mbili, ukumbi wa mikutano na uwanja wa michezo pia vilikuwa karibu na eneo hilo la viwandani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga