1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Changamoto gani zinamkabili Lula da Silva?

9 Januari 2023

Serikali ya Brazil iliyomaliza muda wake imeliacha taifa hilo katika mzozo mkubwa wa kibajeti na kadhia kwa jamii. Tofauti na ilivyokuwa katika kipindi chake cha kwanza, Kulikoni?

https://p.dw.com/p/4Lux1
Brasilien Brasilia | Luiz Inacio Lula da Silva, Präsident | Treffen mit MinisterInnen
Picha: Adriano Machado/REUTERS

Bila shaka huwezi kumlinganisha mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Luiz Inacio Lula da Silva aliyerejea madarakani kama rais Januari Mosi mwaka huu na Lula yule  ambaye alipokea kijiti kutoka kwa rais wa wakati huo Fernando Henrique Cardoso katika eneo lile lile miaka 20 iliyopita. Cardoso wa Social Democrat alimwachia mrithi wake msingi thabiti wa kiuchumi ulimfungulia milango Lula ya kuimarisha ukuaji na kupunguza umaskini.

Mchambuzi wa sayansi ya siasa wa taasisi ya Insper iliyojikita katika mji wa Sao Paulo Carlos Melo ameiambia DW kwamba cardoso alishughulikia changamoto mfumuko wa bei kwa kuongeza viwango muhimu vya riba. Lakini Jair Bolsonaro wa siasa kali za mrengo wa kulia ameliacha taifa hilo katika mzozo mkubwa wa kibajeti na mahusiano tete na bunge, amesema mchambuzi huyo.

Na wakati changamoto ni kubwa hata zaidi, anasema Melo na kuongeza kuwa Lula atalazimika kuisawazisha bajeti, hatua ambayo pia itamlazimu kuchukua mkondo mpya na hasa atakapotakiwa kulishawishi bunge kwa sababu anahitaji fedha na kupitisha sheria mpya, ambavyo vinatakiwa kupitishwa na bunge.

Hata hivyo, kambi ya mrengo wa kulia bungeni ilijiimarisha katika uchaguzi wa mwezi Oktoba. Wafuasi wa Bolsonaro na vyama vinavyojiita vya mrengo wa Katikati vilipata  wingi wa kutosha bungeni na hapo ndipo hasa Lula atalazimika kusaka makubaliano, hii ikiwa ni kulingana na mchambuzi huyo.

Brasilien Brasilia 2019 | Jair Bolsonaro, Präsident & Edir Macado & Silvio Santos
Rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro(katikati) akiwa katika moja ya dhifa wakati akiwa rais wa taifa hilo.Picha: Evaristo Sa/AFP/Getty Images

Kwenye kampeni za uchaguzi, Lula aliahidi kukabiliana na bajeti ambazo haziko wazi. Na katika kisa chochote, atalazimika kufanya makubaliano na spika wa bunge mwenye ushawishi mkubwa, Artur Lira. Mwaka 2015, mrithi wake Dilma Rousseff alijikuta katika mkwamo wa kimamlaka na spika wa wakati huo Eduardo Cunha, ambaye pia alihusika katika mchakato wa kumuondoa Rousseff.

Lula da Silva anakabiliwa na mazingira mapya ya kisiasa, yatakayompa changamoto.

Mazingira ya sasa ya kisiasa hayawezi kulinganishwa na ya mwaka 2003, anasema Marco Antonio Teixeira, mtaalamu mwingine wa sayansi za siasa kutoka taasisi ya FGV na kuongeza kuwa ni kwa sababu hata matokeo ya uchaguzi pia yako tofauti.

Mwishoni mwa mwaka 2002, Lula alishinda kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura, lakini Oktoba mwaka jana, alipata asilimia 50.9 tu, hii ikimaanisha kwamba upinzani kwa sasa ni mkubwa, amesema Taixeira, bila kusahau kuzungumzia kashfa ya rushwa iliyomtia hatiani na kuhukumuiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela. Ingawa, hukumu hiyo ilibatilishwa lakini kimemshushia hadi Lula, mbele ya macho ya waBrazil.

Brasilien Lula gewinnt die Wahl knapp
Raia nchini Brazil wanasubiri kuona mabadiliko katika nyanja tofauti nchini humo yatakayoletwa na Brazil.Picha: Caio Guatelli/AFP

Anasema Lula atalazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, itakayokutanisha wanasiasa kutoka pande zote za kisiasa na kuongeza kuwa chama chake cha Wafanyakazi, PT kiliidhibiti serikali mwaka 2003 lakini sasa anajaribu kushirikishana na pande nyingine kama chama cha mrengo wa kulia cha Uniao Brasil.

Soma Zaidi: Baraza la seneti nchini Brazil lambana Bolsonaro

Mchambuzi huyo anasema Lula ni lazima achukue hatua za haraka. Teixeira hata hivyo anakiri kwamba haitakuwa rahisi. Anasema Brazil kwa sasa inakabiliwa na mzozo wa kiuchumi ambao ni mbaya zaidi ya ule wa mwaka 2002 ingawa kwa upande mwingine anasema hali imeimarika kiasi katika miezi ya karibuni.

Lakini kwa upande wa kimataifa, huenda kukashuhudiwa mafanikio ya haraka. Taswira ya Bolsonaro kuhusiana na mazingira na haki za binadamu ni dhaifu sana mbele ya jukwaa la kimataifa, na kwa maana hiyo, kuchaguliwa kwa Lula kunaipa Brazil nafasi zaidi duniani, anasema Teixeira, akiangazia zaidi hatua ya Lula ya kushiriki mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP27 nchini Misri mnamo Novemba, akisema huo ulikuwa ni ujumbe mzito.

Amesema, iwapo Lula atafanikiwa kufanya maboresho ya haraka Brazil inaweza kupata uwekezaji mkubwa wa kigeni na hasa katika ulinzi wa mazingira na uchumi endelevu.