1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League Barca uso kwa uso na Leverkusen

Sekione Kitojo16 Desemba 2011

Kinyang'anyiro cha mabingwa wa Ulaya , Champions League kinaingia katika duru ya mtoano mwakani , wakati timu 16 bora zitawania taji hilo wakati Barcelona ikiumana na Bayer Leverkusen ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/13UXm
Bildmontage. Quelle: Manchester United's Wayne Rooney leaves the field after the Champions League Group C soccer match against Basel at the St. Jakob-Park stadium in Basel, Switzerland, Wednesday, Dec. 7, 2011. (Foto:Keystone/Peter Klaunzer/AP/dapd) Manchester City's Gareth Barry reacts against Bayern Munich during their Champions League group A soccer match at the Etihad Stadium, Manchester, England, Wednesday Dec. 7, 2011. (Foto:Tim Hales/AP/dapd)
Wayne Rooney wa Manchester United ataonekana sasa katika Europa League.Picha: dapd/DW-Montage

Mabingwa watetezi Barcelona watatoana jasho na Bayer Leverkusen wakati Bayern Munich ambayo inapigiwa upatu msimu huu kutoroka na taji la champions League inakumbana na Basel ya Uswisi katika duru ya mtoano ya timu 16 katika Champions League.

Mabingwa mara saba wa kombe la mabingwa wa Ulaya AC Milan inakumbana na Arsenal London ikiwa ni mmoja kati ya mpambano kati ya timu za Uingereza na Italia, wakati Napoli ikiwa na miadi na Chelsea.

Arsenal imefanikiwa kusonga mbele katika mapambano yote manane wakati ilipopata upinzani kutoka Italia katika duru ya mtoano.

Iwapo tutaendelea kuwa makini na kucheza kwa nguvu zote , tutakuwa na nafasi ya kuingia katika duru ya robo fainali, amesema afisa mkuu wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge, katika tovuti ya klabu hiyo . Lakini aliwatahadharisha wachezaji wake kwa kusema tafadhalini msiwadharau Basel. Timu hiyo kutoka Uswisi inakumbana na Bayern.

Fainali ya msimu huu wa Champions League itafanyika mjini Munich katika uwanja wa Allianz Arena mwezi Mei.

Miongoni mwa timu nne za Uingereza zilizokuwamo katika kinyang'anyiro hiki cha Champions League ni mbili tu zimenusurika . Chelsea na Arsenal zote za mjini London na kuziacha Machester United na Manchester City kutumbukia katika ligi ya Ulaya.

Wakati huo huo, Manchester United itajitupa uwanjani kwa mara ya kwanza kuwania ubingwa wa kombe la Ulaya katika Europa League dhidi ya mabingwa mara nne wa kombe la mabingwa wa Ulaya, Ajax Amterdam, mwakani baada ya vilabu vya Uingereza kupangwa na timu machachari jana Ijumaa.

Adhabu ya United kutolewa na mapema kwa fedheha katika duru ya kwanza ya msimu huu wa champions League ni mpambano dhidi ya vigogo wa soka nchini Uholanzi, Ajax Amsterdam, ambao wanajivunia historia ya mafanikio katika soka la Ulaya . Timu hizo mbili ziliwahi kukutana katika kombe la zamani la UEFA katika msimu wa mwaka 1976/77, United ikisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-1.

Mshindi wa mpambano huo huenda akakutana na ama Lokomotiv Moscow ama Athletic Bilbao katika kundi la timu 16 bora. Mahasimu wakuu wa Manchester United katika Premier League , Manchester City wakati huo huo wamepangwa katika mpambano ambao utawachukua hadi nchini Ureno kukumbana na mabingwa watetezi wa kombe hilo FC Porto. Na iwapo City wanahimili vishindi vya Porto huenda isiwe safari yao ya mwisho kwenda Ureno. Huenda wakapambana na Sporting Lisbon ama na Legia Warsaw katika kundi la timu 16 bora.

Schalke 04 imepangwa dhidi ya Viktoria Plzen , Hannover 96 mpinzani wake ni Club Bruges ya Ubelgiji.

Meneja wa Chelsea, Andre Villas-Boas, amekiri kuwa hafahamu hali ya baadaye ya mshambuliaji kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, Didier Drogba, kwa kuwa hali yake ya kubaki katika timu hiyo bado haijaamuliwa, lakini amesisitiza kuwa Fernando Torres haendi kokote.

Uwezekano wa washambuliaji hao wawili kubaki na klabu hiyo imeingia katika hali ya wasi wasi wakati Drogba akisemekana kuwa huenda akajiunga na mwenzake Nicolas Anelka huko China wakati pia kumekuwa na fununu kuwa Chelsea huenda ikapunguza mzigo wa hasara kwa kuachana na Torres.

Lakini Villas-Boas amesisitiza kuwa ana shauku ya kuwabakiza washambuliaji wote wawili katika kikosi cha Stamford Bridge. Drogba mwenye umri wa miaka 33 ametokea kuwa chagua la kwanza la Villas-Boas katika ushambuliaji katika hatua ya Chelsea ya kufufuka hivi karibuni, lakini mkataba wake unaisha mwishoni mwa kampeni ya msimu huu.

Kocha wa Manchester United, Sir Akex Ferguson, ameondoa uwezekano wa kufanya manunuzi katika dirisha dogo la majira ya baridi , mwezi Januari, licha ya kuongezeka kwa mzozo wa majeruhi katika klabu hiyo. Mchezaji wa kiungo Darren Fletcher wiki hii alikuwa mmoja kati ya wachezaji lukuki ambao ni majeruhi katika kikosi cha Sir Alex, ambapo ni pamoja na nahodha Nemanja Vidic , ambaye hatakuwamo kikosini hadi msimu huu kwisha, pamoja na mshambuliaji hatari Javier Hernandez Chicharito.

Nayo Everton imefikia makubaliano kimsingi ya kumrejesha mshambuliaji wa kimataifa wa Marekani Landon Donovan katika Premier League kwa mkataba wa muda mfupi kutoka LA Galaxy.

FC Barcelona jana Ijumaa walikuwa wakitathmini gharama za kombe la dunia la vilabu baada ya kumpoteza mshambuliaji David Villa baada ya kuvunjika mguu ambapo atakaa nje ya uwanja kwa takriban miezi mitano.

Kuumia kwa Villa kulitokea muda mfupi kabla ya mapumziko katika mchezo wake wa nusu fainali dhidi ya Al Sadd ya Qatar, ambapo mabingwa hao watetezi waliicharaza timu hiyo kutoka Qatar kwa mabao 4-0. Boss wa Barca Pep Guardiola sasa anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwaweka vijana wake kuweka mawazo yao yote katika soka.

Timu hiyo ya Katalunia inakabiliwa na kibarua kigumu katika mchezo wa fainali hapo kesho Jumapili dhidi ya mabingwa wa America ya kusini Santos kutoka Brazil.

Pep Guardiola ambaye katika muda wa miaka mitatu akiwa kocha wa Barcelona ameshinda kila taji alimoshiriki , amekiri kuwa vijana wake wametaharuki , baada ya kuumia kwa Villa usiku wa alhamis, ambapo aliumia wakati alipoanguka vibaya na mara moja aliashiria kupata msaada kutoka benchi la ufundi.

Wachezaji wamefadhaika. Upotevu kama huu unakuacha ukiwa mgonjwa , huna raha, pamoja na kuwa na ombwe la mawazo. Kila mmoja anajiweka katika nafasi yake na anafahamu jinsi atakavyojisikia vibaya. Lakini Barcelona inafahamu kuwa ni changamoto ya aina yake wakati watakapopambana na Santos.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre

Mhariri: Miraji Othman

Mhariri : Othman Miraji