1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha upinzani Uingereza,Labour,chaingia kwenye mpasuko

9 Mei 2021

Mpasuko na mivutano ndani ya Labour umekuja baada ya chama hicho kufanya vibaya sana katika chaguzi za bunge na mabaraza ya miji zilizofanyika nchini Uingereza

https://p.dw.com/p/3tAJT
Großbritannien Labour-Chef Keir Starmer
Picha: Jessica Taylor/UK PARLIAMENT/AFP

Chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza cha Labour kimegawika kuhusu mkakati wake wa baadae na chama hicho kujikuta kimetumbukia kwenye mvutano wa kisiasa wa wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama chao. Ni baada ya chama hicho kufanya vibaya sana katika chaguzi zilizofanyika nchini humo.

Keir Starmer kiongozi wa Labour tangu mwaka 2020 alimtimua mwenyekiti wa chama hicho Angela Rayner siku ya Jumamosi jioni baada ya kusema amevunjwa moyo sana na matokeo ya uchaguzi.

 Inasemekana kwamba kiongozi huyo wa Labour ameshajiandaa kufanya mageuzi ya baraza lake kivuli  wakati ambapo etieti zikiongezeka kuhusu hatma yake yeye mwenyewe binafsi kama kiongozi.Gazeti la Times liliandika kwamba mageuzi ya Starmer huenda anapanga kuyafanya mwanzoni kabisa mwa wiki ijayo na pengine hata Jumatatu.

UK London | Lord Dubs engagiert sich in Flüchtlingshilfe
Picha: Wiktor Szymanowicz/NurPhoto/picture alliance

Wafuasi wa kiongozi aliyepita wa chama hicho Jeremy Corbyn walisikika wakimkosoa Starmer ambapo mshirika wa karibu kabisa na Corbyn,ambaye ni mbunge wa chama hicho cha Labour Diane Abbott amekiambia kituo cha televisheni cha Sky kwamba kwa namna nyingi matokeo ya uchaguzi yamewavunja moyo.

Na akaongeza kusema kwamba hatua iliyochukuliwa ya kumtimua mwenyekiti Angela Rayner haikuwa ya busara.  Sio Abbott tu aliyetoa kauli ya kumkosoa kiongozi wa chama chake lakini hata John McDonnell, aliyewahi kuwa waziri kivuli wa fedha wakati chama cha Labour kikiongozwa na Corbyn akihojiwa na  shirika la habari la uingereza BBC amemkosoa Starmer kwa kushindwa kuunda sera za kuvutia.

Mwanasiasa huyo amesema huwezi kumpeleka mgombea kwenye kinyang'anyiro akiwa mweupe hana kitu, bila ya sera. Lakini ikumbukwe kwamba chini ya Corbyn chama hicho cha Labour kiliharibiwa na tuhuma za kuwa na misimamo ya chuki dhidi ya wayahudi na matokeo yake kikaishia kufanya vibaya sana katika uchaguzi mkuu 2019.

Mnamo Aprili chama hicho kikamchagua Starmer kuwa kiongozi wake.Starmer alikuwa ni wakili wa kutetea haki za binadamu na mkurugenzi mwendesha mashtaka wa umma.Alichaguliwa kukiongoza chama hicho kwa ahadi kwamba atakirudisha kwa wapiga kura.Lakini uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita umeonesha kwamba kwa hilo hakufanikiwa,hata chembe.

Labour ilifanya vibaya sana katika uchaguzi wa mabaraza ya miji uliofanyika alhamisi huko England na kushindwa na wahafidhina,katika uchaguzi muhimu wa marudio huko Hartlepool,Kaskazini mashariki mwa England,eneo ambalo tangu miaka ya 1970 ni ngome hasa ya chama hicho cha Labour.

Großbritannien Hartlepool | Jill Mortimer
Mgombea wa Conservative-Hartlepool Jill MortimePicha: Ian Forsyth/Getty Images

Huko Scotland, Labour ambayo inaongozwa na Anas Sarwar tangu Februari mwaka huu,kilishindwa kutetea viti viwili katika uchaguzi wa bunge la huko wakati  kikipata mafanikio huko Wales na kuendelea kushikilia uongozi wa bunge la huko pamoja na viti vingi vya nafasi ya meya ikiwemo London ambako Sadiq Khan ameshinda muhula wa pili.

Na meya maarufu huko Manchester,kaskazini mwa Uingereza,Andy Burnham aliyerudi kiulaini anaonesha  wazi kusababisha changamoto katika uongozi wa Starmer katika chama hicho cha Labour.Meya huyo ameshasema kwamba ikiwa chama kinahisi kinamuhitaji basi yupo tayari.

England Andy Burnham
Picha: Jacob King/empics/picture alliance

Kwa upande mwingine matokeo ya uchaguzi ya Uingereza yanaonesha kuwa ni kura ya imani na uongozi wa Boris Johnson baada ya kujitoa Umoja wa Ulaya na hatua ya nchi ya kufanikiwa katika zoezi la kutoa chanjo licha ya idadi ya vifo nchini humo kubakia kuwa ya juu kabisa ikilinganishwa na nchi za barani Ulaya.

Waziri mkuu Boris Johnson amewaalika viongozi wa Scotland kwenye mazungumzo ya dharura kuhusu muungano  baada ya chama tawala cha Scotland  SNP kinachopigania Scotland ijitenge,kushinda uchaguzi wa bunge kwa mara ya nne mfululizo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sudi Mnette

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW