1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha SPD bado kinaongoza kwenye kura ya maoni

23 Septemba 2021

Zikiwa zimesalia siku tatu tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Ujerumani, idadi ya wapiga kura ambao bado hawajaamua ni nani wa kumpigia kura imepungua.

https://p.dw.com/p/40kzy
SPD Parteitag 2002 | Olaf Scholz und Gerhard Schröder
Picha: Enters/imago images

Zikiwa zimesalia siku tatu tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Ujerumani, idadi ya wapiga kura ambao bado hawajaamua ni nani wa kumpigia kura imepungua, na kuongeza shinikizo zaidi kwa chama cha kihafidhina cha Angela Merkel, Christian Democratic Union CDU, kinachojaribu kupunguza mwanya wa uongozi wa chama cha Kisoshalisti cha SPD kwa mujibu wa kura ya maoni. 

Kwa mujibu wa mtandao wa YouGov uliowahoji wapiga kura wa Ujerumani kuelekea kwa uchaguzi wa Septemba 26, ni kuwa asilimia 74 ya wapiga kura tayari wameamua ni chama gani watakachokipigia kura.

Soma pia: Uchaguzi wa Ujerumani: Merkel asema CDU ina mlima wa kupanda

Katika kura ya maoni iliyotolewa leo Alhamisi, asilimia 15 ya waliohojiwa wamesema watafanya uamuzi wao wa mwisho kuhusu nani wa kumpigia kura hapo baadaye, asilimia 9 ya watu hawakuweka bayana ni nani watakayempigia kura wakati asilimia moja wakisema hawajui watampigia nani.

Kura za maoni za awali zilionyesha kuwa asilimia 30 au hata pengine asilimia 40 ya wapiga kura walikuwa bado hawajaamua ni chama gani watakachokipigia kura, hoja iliyotolewa pia na mgombea wa Ukansela kupitia chama cha kijani Annalena Baerbock.

Ama kuhusu umaarufu wa vyama vya kisiasa kuelekea kwa uchaguzi huo, mwanya wa uongozi wa chama cha Kisoshalisti SPD umepungua kwa alama nne tu mbele ya chama cha Christian Democratic Union CDU.

Umaarufu wa chama cha SPD umepungua

Armin Laschet, Kanzlerkandidat der CDU
Armin Laschet, mgombea wa Ukansela kwa tiketi ya chama cha CDUPicha: DW

Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na kampuni ya takwimu ya Kantar ni kuwa umaarufu wa mgombea Ukansela kwa tiketi ya chama cha SPD Olaf Scholz umepungua kwa alama moja, hadi asilimia 25 wakati uungwaji mkono wa vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU ambaye mgombea wake wa Ukansela ni Armin Laschet umeongezeka kwa alama moja, hadi asilimia 22.

Chama cha kijani kimepoteza pointi moja hadi asilimia 16 huku chama cha kutetea uhuru wa biashara cha FDP kikipata asilimia 11, wakati chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kikipata asilimia 12 nacho kile chenye kuegemea siasa za mrengo wa kushoto cha Die-Linke kikipata asilimia 7.

Soma pia: Uchaguzi wa Ujerumani: Ni upi urathi wa sera ya kigeni ya Merkel?

Armin Laschet amesema, "Natambua jukumu zito la ofisi ya Kansela. Nitafanya kila niwezalo ili tushirikiane pamoja, tusimamie uchaguzi ujao vizuri na kuhakikisha kuwa vyama ndugu vya muungano wa CDU na CSU, vinatoa Kansela ajaye."

Merkel ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005, ataachia ngazi nafasi yake kama Kansela wa Ujerumani baada ya uchaguzi wa Jumapili huku mgombea wa SPD Olaf Scholz akionekana kuwa chaguo la wapiga kura wengi.

Ingawa utafiti wa kura za maoni hauchori picha halisi ya jinsi matokeo ya uchaguzi wenyewe utakavyokuwa, umaarufu wa vyama hivyo umesalia jinsi ulivyo sasa tangu mwezi Agosti.

Uchaguzi wa Jumapili unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, wakati kukiwa na wasiwasi wa chama cha Merkel kung'olewa madarakani baada ya kushika usukani wa kuliongoza taifa kwa karibu miaka 16.