1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurundi

Chakula cha msaada kupunguzwa kwa wakimbizi Burundi: WFP

Amida Issa31 Machi 2023

WFP limepunguza kwa asilimia 50 msaada wa chakula unaotolewa kwa wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walioko kwenye kambi za Burundi na wale wakimbizi wa Burundi waliorejea kutoka kwenye nchi walizokimbilia

https://p.dw.com/p/4PZ5l
Burundi kongolesische Flüchtlinge in Rumonge
Picha: DW/A. Niragira

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limepunguza kwa asilimia 50 msaada wa chakula unaotolewa kwa wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walioko kwenye kambi za Burundi na wale wakimbizi wa Burundi waliorejea kutoka kwenye nchi walizokimbilia wakiwa katika vituo kwa kusubiri kuelekea kwenye maeneo yao ya asili. . Hatua hiyo inaanza kuchukuliwa kesho Jumamosi.

Claude Kakule, Naibu Mkurungenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, amethibitisha hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza kwa asilimia 50 msaada wa chakula uliokuwa ukitolewa kwa wakimbizi wa Kongo walio katika kambi za Burundi na wale wakimbizi wa Burundi waliorejea kutoka kwenye nchi walizokimbilia.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi habari, Kakule amesema hatua hiyo imetokana na sababu kadha zilosababisha WFP kutoweza kupata pesa zinazohitajika ili kuwapatia msaada wa chakula wakimbizi elfu 56.

Wakimbizi waishio Tanzania watakiwa kurejea Burundi

Kulingana na Kakule, sababu hizo ni pamoja na athari za vita vya Ukraine, athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuongezeka kwa nchi nyingi ambazo zinahitaji msaada wa chakula.

''Kama mnavyojuwa mwaka huu fedha tutakazopewa zitapungua kutokana na vita vya Ukraine, janga la COVID-19, nchi nyingi zakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, familia nyingi haziwezi kujitosheleza kwa chakula. Mahitaji ya kiutu yameongezeka na wafadhili wamelazimika kujaribu kuzisaidia nchi nyingi. Msaada utaendelea kupunguzwa hadi pale tutakapopata Dola milioni 7 zinazohitajika.''

Naibu huyo mkurugenzi wa WFP amekiri kuwa kupunguwa kwa msaada wa chakula kutoka katika shirika lao kutawaathiri watoto, wanawake wajawazito na wazee ambapo watalazimika kula mloo mmoja badala ya milo mitatu kama ilivyokuwa awali.

''Wakimbizi walioko makambini hawana njia nyingine ya kununuwa chakula, hivyo watalazimika kupunguza mlo, hali inayohatarisha usalama wao wa chakula na bila shaka itawaathiri watoto, wanawake, wajawazito, na wazee.''

Afisa huyo wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani amebainisha kuwa walijaribu kuwasiliana na mashirika mengine yanaohudumu katika kuwashughulikia wakimbizi, lakini hawakufanikiwa. Amesema kwamba wataendelea kutafuta wafadhili wengine ili kuziba pengo hilo la dola milioni 7 zinazohitajika.

Burundi imewapa hifadhi wakimbizi elfu 99 wengi wao wakiwa kutoka DRC, na vita

vya hivi karibuni kati ya majeshi ya serikali na waasi wa M3 vimesababisha idadi ya wakimbizi kutoka maeneo ya mashariki mwa Kongo kuongenzeka.

Shirika la WFP, limepunguza kwa asilimia 50 msaada wa chakula kwa wakimbizi wakati Burundi ikabiliwa na mfumuko wa bei za mahitaji ya vyakula.

Amida ISSA, DW, BUJUMBURA.