1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAIRO Magdy Elnashar hana uhusiano na kundi la al-Qaeda

16 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEu6

Maofisa nchini Misri wamesema Magdy Elnashar, aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika mashambulio ya mabomu mjini London Uingereza, hana uhusiano wowote na kundi la kigaidi la al-Qaeda. Wamesema pia kwamba mtuhumiwa huyo amekanusha kuhusika kwenye mashambulio hayo.

Polisi walimkamata Elnashar katika uwanja wa ndege wa Cairo Alhamisi iliyopita. Habari zilizotolewa na vyombo vya habari zimemueleza jamaa huyo kama mtaalamu wa biokemia aliyesomea nchini Marekani na ni mwanafunzi wa shahada ya udaktari katika chuo kikuu cha Leeds nchini Uingereza.

Wakati huo huo, Pakistan imetangaza kwamba imewakamata wanaume wanne wanaoshukiwa kuhusika katika mashambulio ya London. Mmoja wa magaidi hao waliojilipua alikuwa amekutana na mpakistani aliyetiwa mbaroni kwa kulipua kanisa mjini Isalamabad mnamo mwaka wa 2002.