1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi kudai fidia kutoka kwa Ujerumani na Ubelgiji

17 Agosti 2020

Ripoti za vyombo vya habari zinaarifu kuwa Burundi inazitaka Ujerumani na Ubelgiji ziilipe euro bilioni 36 kama fidia za ukoloni wao.

https://p.dw.com/p/3h4ce
Neuer Präsident von Burundi, Evariste Ndayishimiye
Picha: DW/A. Niragira

Baraza la seneti la nchi hiyo limeunda jopo la wataalam watakaochunguza madhara yaliyotokana na ukoloni na kushauri kuhusiana na kiasi cha fidia.

Kituo cha redio cha Ufaransa RFI kinasema mara tu kiasi cha fidia kitakapoamuliwa Burundi inapanga kupeleka mapendekezo hayo kwa serikali za Ujerumani na Ubelgiji. Nchi hiyo pia inapanga kuitisha turathi zake za kihistoria zilizoibwa, kutoka kwa nchi za Ulaya.

Burundi ilikuwa koloni la Ujerumani kutoka 1890 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia nchi hiyo ikawa koloni la Ubelgiji mpaka ilipopata uhuru 1962. katika enzi za ukoloni, nchi hizo zilichochea mgawanyiko kati ya Wahutu na Watutsi.

Oberstes Gericht Burundi
Jengo la Mahakama ya Juu ya BurundiPicha: DW/A. Niragira

Jambo hili lilichangia kuzuka kwa mapigano mabaya baina ya makabila hayo mawili katika miaka ya 1970 na mapigano mengine ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka 12 kuanzia 1993. Karibu watu laki tatu walifariki dunia katika mapigano hayo.

Serikali ya Ubelgiji ilikuwa na mpango wa kuwateka nyara watoto kutoka Burundi na Congo katika miaka ya 1940 na 1950. Mwaka 2009, Ubelgiji iliomba msamaha rasmi kwa vitendo hivyo.

Ingawa haijulikani sana katika masuala ya ukoloni, Ujerumani wakati mmoja ilikuwa ndiyo nguvu ya nne kubwa zaidi ya ukoloni duniani. Pamoja na eneo lililoitwa German East Africa lililojumuisha Rwanda na sehemu za Tanzania pamoja na Burundi, Ujerumani ilikuwa na maeneo mengine pia kama nchi ambazo sasa ni Ghana na Namibia.

Serikali ya Ujerumani imekuwa katika meza ya mazungumzo na Namibia tangu 2015 kwa kuwa nchi hiyo inataka fidia ya fedha pamoja na kuombwa msamaha rasmi na Ujerumani kwa hasara iliyopata na uhalifu uliofanywa katika kipindi cha ukoloni.

Ubelgiji inapanga kuunda jopo la wataalam kuishauri serikali kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na historia yake ya kikoloni.

(DW https://bit.ly/3h41qWD)