1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buriani Mzee Moi

11 Februari 2020

Wakenya wa matabaka mbalimbali wamejumuika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo kwa ajili ya ibada ya wafu ya aliyekuwa Rais Hayati Daniel Toroitich Arap Moi.

https://p.dw.com/p/3XaRE
Kenia Begräbnis Daniel Arap Moi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Kuanzia alfajiri, makumi ya Wakenya walianza kumiminika katika uwanja huo huku kukiwepo ulinzi mkali.

Jeneza la Moi lililofunikwa kwa bendera ya Kenya, lilibebwa kuanzia Ikulu ya Rais hadi uwanja huo wa Nyayo, safari ya umbali wa kilomita tano.

Ibada hiyo ya wafu ilitarajiwa kuanza mwendo wa saa nne asubuhi punde tu baada ya kuwasili Rais Uhuru Kenyatta pamoja na wageni wengine mashuhuri wakiwemo Marais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde, Paul Kagame wa Rwanda, Salva Kiir wa Sudan Kusini na Yoweri Museveni wa Uganda.

Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilitangaza kuwa leo Jumanne itakuwa siku ya mapumziko.

Mwili wa Mzee Moi uliwekwa katika majengo ya bunge tangu Jumamosi na kutoa fursa kwa watu kutoa heshima zao za mwisho.

Jumatano, kutafanyika ibada nyengine katika chuo kikuu cha Kabarak kabla ya mwili wake kuzikwa nyumbani kwake Kabarak.

Rais huyo wa pili wa Kenya alifariki dunia Februari 4, wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 95. Moi aliaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali ya Nairobi. Aliongoza Kenya kwa kipindi cha miaka 24 kuanzia mwaka 1978 hadi 2002 alipoachia madaraka.

Vyanzo /Reuters/AFP