1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUNIA : Umoja wa Mataifa yaaga wanajeshi wake waliouwawa

27 Februari 2005
https://p.dw.com/p/CFar

Kikosi cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo MONUC hapo jana kilitowa heshima zake kwa wanajeshi 9 wa kulinda amani kutoka Bangladesh waliouwawa baada ya kuvamiwa na kikosi cha wanamgambo katika jimbo la kaskazini mashariki la Ituri.

Mkuu wa kikosi hicho cha MONUC Dominique MacAdams akitowa heshima zake kwenye utaratibu wa kuwaaga wanajeshi hao waliopoteza maisha katika mji mkuu wa Ituri Bunia amekaririwa akisema kwenye mikono ya maadui wa amani maisha ya binaadamu hayana thamani.

Mapema hapo jana bendera za Bangladesh na Umoja wa Mataifa zilipepea nusu mlingoti katika kutowa heshima kwa wanajeshi hao waliouwawa wakiwa kazini kama sehemu ya wanajeshi 14,500 walioko nchini humo kusaidia kurudisha amani katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati ilioharibiwa na vita vya mwaka 1998 hadi mwaka 2003.

Hapo Ijumaa kundi la watu wasiojulikana lenye silaha lilishambulia msafara wa wanajeshi hao wa kulinda amani na kuwauwa 9 pamoja na kujeruhi wengine 11.

Hilo ni shambulio baya kabisa kuwahi kufanywa dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilioko Congo.