1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Bunge Marekani lashindwa kumpata spika kwa siku ya pili

5 Januari 2023

Baraza la Wawakilishi nchini Marekani lenye mpasuko mkubwa limetumbukia katika mzozo kwa siku ya pili mfululizo jana baada ya duru mpya za upigaji kura kushindwa kumpata mshindi wa kinyang'anyiro cha uspika

https://p.dw.com/p/4Lkb7
USA US-Repräsentantenhaus Wahlen Kevin McCarthy
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Warepublican katika Baraza la Wawakilishi walishindwa kwa siku ya pili mfululizo kumchagua kiongozi, wakati kundi la wahafidhina chamani likiendelea kukaidi wito wa Rais wa zamani Donald Trump wa kuungana nyuma ya mshirika wake Kevin McCarthy.

Soma pia: Wabunge wa Marekani kujaribu tena kuchagua Spika

Baada ya kushindwa katika duru tatu za upigaji kura na mikutano kadhaa ya faragha, McCarthy alionekana kuwa mbali kuchukua wadhifa wa spika wa bunge, wadhifa wenye nguvu kubwa ambao ni wa pili baada ya makamu wa rais katika kurithi ofisi ya rais.

USA Kat Cammack
Picha: Jack Gruber/USA TODAY Network/IMAGO

McCarthy anayetokea California alishindwa katika duru ya nne, ya tano na ya sita ya uchaguzi wa kuwa spika. Alipata kura 201 pekee kati ya 218 zinazohitajika, wakati Warepublican 20 wakimpigia kura jana Mjumbe Byron Donalds, Merepublican aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2020. Mrepublican mmoja alikataa kumuunga mkono mgombea yeyote. Wademocrat wote 212 walimpigia kura Jeffries. Akizungumza wakati akimpigia McCarthy kura, Mrepublican Kat Cammack wa Florida alisema mambo kwa sasa ni magumu. "Kwa Wamarekani wote wanaotazama hivi sasa. Nataka kuwaambia kwamba tunawasikia. Tunawasikia. Na mara hii tutalipatia. Haijalishi mchakato huu umevurugika kiasi gani, tutaibuka tukiwa bora zaidi kwa kuyapitia haya kwa sababu halkuna kitu kizuri kinachokuja kwa urahisi." Alisema Cammack.

Wapinzani walisema vita hivyo vya uongozi huenda vikaendelea kwa wiki kadhaa. Wabunge kisha walipiga kura kwenda nyumbani jioni na kujaribu tena leo mchana.

Bunge la Marekani litafanikiwa kutegua kitendawili cha spika?

Mkwamo huo unaibua maswali kuhusu uwezo wa Warepublican kuongoza katika miaka miwili ijayo wakati wakionekana kuyumba katika kile ambacho kimsingi huwa kura ya kawaida mwanzoni mwa vikao vya bunge.

Soma pia: Baraza la Wawakilishi Marekani lashindwa kuchagua spika

Bunge lazima kwanza limchague kiongozi kabla ya kuwaapisha wajumbe na kuanza shughuli za bunge.

Uwezekano wa Bunge kumchagua spika Mrepublican kupitia msaada wa Wademocrat ulionekana kushika kasi.

Mdemocrat anayekumbatia mawazo mapya Ro Khanna anasema anaweza kumuunga mkono Mrepublican mwenye msimamo wa wastani anayeweza kukubali kushirikiana na Wademocrat kuhusu ufadhili wa serikali na ukomo wa madeni.

Kiongozi wa Wademocrat bungeni Hakeem Jeffries aliwaambia waandishi wa Habari kuwa Warepublican hawajawaomba Wademocrat kuhusu chaguo hilo.

AFP/Reuters