1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lamthibitisha Mpango kuwa Makamu wa rais Tanzania

30 Machi 2021

Hatimaye Tanzania imempata makamu wa Rais, ambaye ni daktari Philip Isdor Mpango baada ya jina lake kupendekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kisha kupigiwa kura na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

https://p.dw.com/p/3rN5K
Tansania Philip Mpango, Finanzminister
Picha: DW/S. Khamis

Awali hali ya utulivu ilitawala ndani ya ukumbi wa Bunge mara baada ya spika Job Ndugai kuruhusu mpambe wa rais Kuingia ukumbini na kuwasilisha bahasha yenye jina lililopendekezwa la makamu wa Rais, huku spika Ndugai akipokea bahasha hiyo na kulitangaza jina hilo.

"Muheshimiwa rais anasema muheshimiwa spika, nawasilisha bungeni jina la muheshimiwa Philip Isdor Mpango kwa nafasi ya makamu wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Sasa waheshimiwa wabunge kanuni zetu za bunge hazijatoa muongozo wa namna ya kuthibitisha uteuzi wa makamu wa rais. Hivyo kwa mamlaka niliyopewa kwa kanuni ya tano, natumia uzoefu wa jambo kama hili lililofanyika tarehe 13 Julai 2001, kuthibitisha uteuzi wa makamu wa raisi. Mtakumbuka 2001 baada ya muheshimiwa Omar Ali Juma kuwa amefariki wakati tunamthibitisha muheshimiwa Dkt Shein, tutafuata utaratibu huo wa wakati huo, kwanza nitamuomba muheshimiwa Waziri Mkuu atoe hoja fupi tu ya kulitaka bunge lithibitishe uteuzi wa Makamu wa rais," alisema Job Ndugai.

Imara baada ya kulitangaza jina hilo mchakato wa wabunge kulipigia kura ulifanyika na kwa kauli moja wabunge hao walilipitisha kwa asilimia mia moja ya kura zote

Soma zaidi: Rais Samia Suluhu amsimamisha kazi mkurugenzi wa mamlaka ya bandari

Mpango asema hakutegemea kupata nafasi hiyo

Tansania Parlament Dodoma - Parlamentsvorsitzende mit Philip Mpango und Premierminister Kassim Majaliwa
​​​​Makamu wa rais wa Tanzania Dk Philip Isdor Mpango akiwa bungeni Picha: DW/S. Khamis

Akizungumza mara baada ya jina lake kutangazwa bungeni kuwa ndiye makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Philip Mpango amesema hakutarajia kupata nafasi hiyo.

"Ni heshima kubwa sana sikuwahi kuota, wakati naibu wangu hapa anajibu suali nilikuwa nahangaika na mambo mengine ikiwemo na mishahara ya baadhi ya wabunge ambayo ilikuwa haijalipwa mpaka leo asubuhi, nimetoka nje mara kadhaa kujaribu kuhangaika, kwahiyo nimepigwa na butwaa," alisema Dkt Mpango

soma zaidi: Vilio na simanzi wakati wa kuagwa mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania jijini Dar es Salaam

Kabla ya kushika nafasi hiyo ya makamu wa Rais, Daktari mpango alikuwa Waziri wa fedha na mipango nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka sita na pia mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma kupitia chama cha Mapinduzi CCM.

Daktari Mpango ametwaa nafasi hiyo baada ya aliyekuwa makamu wa Rais wakati wa uongozi wa hayati Rais Magufuli Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati Pombe Magufuli na hivyo nafasi ya makamu ya Rais kuwa wazi.

Mwandishi: Deo Kaji Mkomba/Dodoma