1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ukraine laidhinisha mawaziri wapya walioteuliwa

Sylvia Mwehozi
6 Septemba 2024

Bunge la Ukraine limeidhinisha uteuzi wa waziri mpya wa mambo ya nje pamoja na mawaziri wengine walioziba nafasi zilizoachwa wazi kufuatia mawaziri kadhaa kujiuzulu nyadhifa zao.

https://p.dw.com/p/4kKns
Ukraine | Andrii Sybiha
Andrii Sybiha aliyeteuliwa waziri mpya wa mambo ya nje wa UkrainePicha: REUTERS

Bunge la Ukraine limeidhinisha uteuzi wa waziri mpya wa mambo ya nje pamoja na mawaziri wengine walioziba nafasi zilizoachwa wazi kufuatia mawaziri kadhaa kujiuzulu nyadhifa zao. Balozi wa zamani wa Ukraine nchini Uturuki Andrii Sybiha, ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje, akichukua mikoba ya Dmytro Kuleba ambaye alikuwa mmoja ya watu maarufu wa Ukraine katika jumuiya ya kimataifa. Kabla ya uteuzi wake Sybiha alikuwa naibu waziri wa Kuleba tangu mwezi Aprili.

Katika ujumbe wake kwa njia ya vidio, Rais Volodmyr Zelensky amesema kuwa anataka serikali ifanye kazi zaidi na washirika wa Magharibi wa Ukraine na wawekezaji na kusaidia wanajeshi walio katika uwanja wa mapambano. Kiongozi huyo anatarajiwa kusafiri kuelekea Marekani baadae mwezi huu akitumai kuwasilisha mkakati wa ushindi kwa Rais Joe Biden.