1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaifanyia mageuzi sheria ya uraia

Angela Mdungu
20 Januari 2024

Bunge la Ujerumani limeidhinisha sheria inayorahisisha kanuni za kupata uraia na kuondoa vikwazo kwa watu kuwa na uraia pacha.

https://p.dw.com/p/4bTVF
Ujerumani |Uraia pacha
Wahamiaji wengi sasa watakuwa na fursa ya kuwa raia wa Ujerumani huku wakishikilia uraia wao wa asili.Picha: Daniel Bockwoldt/dpa/picture alliance

Serikali imetoa hoja kuwa mpango huo utasaidia ujumuishwaji wa wahamiaji na kuwavutia wafanyakazi wenye ujuzi kufanya kazi Ujerumani.

Bunge la Ujerumani lilipiga kura 382 dhidi ya 234 kwa ajili ya kuupitisha mpango huo uliowasilishwa na muungano wa vyama vinavyounda serikali inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz. Wabunge 23 hawakupiga kura.

Sheria hiyo mpya itawafanya watu kuwa na sifa ya kuomba uraia wa Ujerumani baada ya miaka mitano au miaka mitatu ikiwa atakidhi viwango maalumu. Watoto waliozaliwa Ujerumani watakuwa raia moja kwa moja ikiwa mzazi mmoja amekuwa mkaazi kwa miaka mitano, tofauti na minane ya hapo awali.

Ujerumani I Bunge la Ujerumani
Bunge la Ujerumani limeidhinisha mageuzi ya sheria ya uraia na kuruhusu uraia pacha.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma zaidi: Ujerumani yakubali kulegeza sheria za uraia kwa wahamiaji

Vikwazo vya kuwa na uraia pacha navyo vitaondolewa. Kabla ya mageuzi haya watu wengi kutoka nchi zilizo nje ya Umoja wa Ulaya na Uswisi, walitakiwa kuukana uraia wa nchi zao ili kupata Uraia wa Ujerumani.

Asilimia 14 ya wakaazi hawana uraia wa Ujerumani

Serikali inasema kuwa asilimia 14 ya idadi ya watu ambayo ni zaidi ya watu milioni 12 waishio Ujerumani hawana uraia wa Ujerumani na kwamba milioni 5.3 kati ya hao wameishi nchini humo kwa takribani muongo mmoja.

Mwaka 2022 takribani watu 168,500 walipewa uraia wa Ujerumani idadi hiyo ikiwa ni kubwa zaidi tangu mwaka 2002. Idadi hiyo ilichochewa na ongezeko la raia wa Syria waliopata uraia kwa kuasiliwa katika muongo mmoja uliopita.

Ujerumani| Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela Olaf ScholzPicha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance /

Hata hivyo sheria ya sasa inaainisha kuwa, watu wanaopata uraia kwa kuasiliwa wanapaswa kuwa na uwezo wa kujihudumia ingawa kuna msamaha kwa watu waliofika Ujerumani magharibi kama wafanyakazi wageni hadi kufikia mwaka 1974, na wale waliokuja kufanyakazi kwa iliyokuwa Ujerumani Mashariki.

Mageuzi ya sheria hiyo ni moja ya mabadiliko ya kijamii ambayo serikali ya muungano wa vyama vinavyundwa na serikali inayoongozwa na kansela Scholz ilikubaliana kuyafanya wakati ilipoingia madarakani mwaka 2021.