1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Somalia lamchagua spika mpya

28 Aprili 2022

Bunge la Somalia limemchagua mwanasiasa wa muda mrefu kama spika wa baraza la chini huku taifa hilo la Pembe ya Afrika likikaribia kufanikisha uchaguzi wa rais, uliocheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja

https://p.dw.com/p/4AYEg
Somalia Mogadischu | Parlament, neu gewählte Abgeordnete
Picha: Abukar Mohamed Muhudin/Anadolu Agency/picture alliance

Baada ya uchaguzi wa spika wa baraza la juu siku ya Jumanne, wabunge katika baraza la chini wamemchagua Sheikh Adan Mohamed Nur anayejulikana kama Sheikh Adan Madobe kuwa spika wa baraza hilo, katika mchakato uliokamilika majira ya Alfajiri.

Uchaguzi huo ulifanyika katika hema moja mjini Mogadishu lililokuwa na ulinzi mkali kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara  katika wiki za hivi karibuni yanayodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Al shabaab, walioanzisha uasi dhidi ya serikali zaidi ya muongo mmoja uliyopita.

Madobe, aliye na miaka 66, alijipatia kura 163 kati ya kura 252 zilizopigwa. Aliwahi kuwa spika kati ya mwaka 2007 na 2010. Madobe hana ushirika wa karibu na rais Mohamed Abdullahi Mohamed wala Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble, ambao wamekuwa wakizozana katika miezi ya hivi karibuni kuhusiana na mchakato wa uchaguzi na suala la usalama.

soma zaidi: Roble ataka wabunge kulindwa kuelekea uchaguzi Somalia 

Rais Abdullahi Mohammed anayejulikana kama Farmajo alimpongeza Madobe huku akisema katika taarifa yake kwamba anatumai kuchaguliwa kwake ni mwanzo mpya wa mabadiliko yatakayoinusuru Somalia. Siku ya Jumanne Abdi Hashi Abdullahi aliye na miaka 76-alichaguliwa tena kama spike wa bunge la senet.

Hali hiyo inatoa nafasi sasa kwa bunge kuanza mara moja mbio za kutafuta na kukubaliana juu ya tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais. Somalia ilitarajiwa kumchagua rais wake mwaka uliyopita lakini ilishindwa kufanya hivyo kabla ya muda wa Farmajo kumalizika Februari mwaka jana.  

Uchaguzi huo ulicheleweshwa pia kufuatia mchakato mzima kugubikwa na vurugu na mapambano ya kuwania madaraka kati ya rais wa sasa na waziri mkuu Roble.

soma zaidi: Ukosefu wa usalama waongezeka Somalia kuelekea uchaguzi

Farmajo alijaribu kurefusha muhula wake kwa kutumia nguvu, hali iliyosababisha vurugu mjini Mogadishu. Baada ya kukabiliwa na shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa, Farmajo alimchagua Waziri Mkuu Roble kutafuta suluhisho ya hali iliyokuwepo, lakini kuendelea kutoelewana kati ya wawili hao katika masuala tofauti ya uongozi kulisababisha kizingiti kikubwa katika mchakato wa uchaguzi na kuzuka hofu ya taifa hilo ambalo tayari linapambana na uasi wa kundi la Al Shabaab na pia kukabiliwa na baa la njaa kuendelea kuyumba zaidi na kutokuwa na uthabiti wa kisiasa.

Kando na changamoto hiyo, nyengine inayoikodolea macho Somalia ni kumalizika kwa muda wa miaka mitatu wa msaada wa kifedha wa takriban dola milioni 400 kutoka shirika la fedha la kimataifa IMF. Muda huo utamalizika katikati ya mwezi Mei iwapo Somalia haitofanikiwa kuwa na utawala mpya utakaoweza kuidhinisha mageuzi yaliyopangwa.

Chanto: afp/reuters