1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Kenya yaidhinisha polisi kutumwa nchini Haiti

16 Novemba 2023

Bunge la Kenya leo limeidhinisha mpango wa kuwapeleka maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti kusaidia kukabiliana na machafuko yanayoongezeka ya magenge ya uhalifu katika taifa hilo la Karibia.

https://p.dw.com/p/4YtE7
Kenya | Polisi wa Kenya kwenye maandamano mjini Nairobi
Kenya inanuwia kupeleka alau askari 1,000 nchini Haiti kuisaidia nchi hiyo kutuliza machafuko.Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Bunge limeunga mkono mswada uliowasilishwa na Kamati ya bunge ya Utawala na Usalama wa Ndani na kuridhia ombi la serikali kuwatuma maafisa wa usalama nchini Haiti.

Kulikuwa na mjadala mkali bungeni huku wabunge wa upinzani wakiipinga mipango hiyo ya serikali, wakisema inakiuka katiba ya nchi.

Waliouunga mkono mswada huo walisema Kenya ina jukumu la kimaadili na wajibu wa kuisaidia Haiti.

Maswala muhimu katika mjadala huo yalikuwa ni nani atakayeufadhili ujumbe huo na sababu gani zinahalalisha kupelekwa kwa vikosi vya usalama Haiti, ambayo iko umbali wa maelfu ya kilomita kutoka Kenya.

Mahakama ya Juu mjini Nairobi inatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya kesi iliyowasilishwa na mgombea urais wa zamani Ekuru Aukot aliyehoji kuwa ujumbe huo, unaooungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ni kosa na kuwatoa muhanga polisi wa Kenya.