1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS:Mawaziri wa ulinzi wa NATO wakutana

1 Desemba 2003
https://p.dw.com/p/CFwG
Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Kujihami wa mataifa ya Ulaya ya Magharibi NATO wanakutana mjini Brussels leo kwa mazungumzo ya siku mbili ambayo yumkini yakahodhiwa na mpango mpya wa Ulaya kuhusu ulinzi. Kabla ya mkutano huo waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld ameonya dhidi ya hatua za Umoja wa Ulaya kuanzisha kitengo huru cha mipango ya kijeshi na kusema kwamba hakupaswi kuchukuliwa hatua yoyote ile ambayo itauweka hatarini umoja huo wa NATO.Katika mazungumzo hayo mawaziri wa ulinzi pia wanatarajiwa kuidhinisha rasmi uamuzi wa kupunguza karibu nusu kikosi kinachoongozwa na NATO cha kuleta utulivu huko Bosnia Herzegovina hapo mwakani. Mawaziri hao pia wanaweza kuzungumzia hali ya hivi sasa nchini Afghanistan ambapo NATO kuanzia mwezi wa Augusti imechukuwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Usaidizi cha Kimataifa ISAF chenye wanajeshi 5,500.