1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Wafadhili waijadili Burundi

13 Januari 2004
https://p.dw.com/p/CFjp
Wafadhili wa Burundi wanatarajiwa kuanza leo mjini Brussels kikao cha siku 2 cha kujadili hatima ya nchi hiyo ambayo kiongozi wake Domitien NDAYIZEYE anatarajia kuwashawishi kutimiza ahadi yao ya kuipatia msaada wa mamilioni ya Dola ya kusaidia ujenzi mpya baada ya Burundi kukumbwa na vita vya miaka 10. Miongoni mwa wajumbe wanaofuatana na Bwana NDAYIZEYE ni pamoja na Waziri mpya wa mambo ya ndani Simon NYANDWI ambaye ni wa chama kikuu cha waasi wa zamani wa CNDD-FDD waliojiunga na serikali Disemba iliopita baada ya kusaini mapatano ya kusitisha mapigano na serikali ya mpito ya Burundi. Baada ya Ubelgiji, Rais NDAYIZEYE atakwenda Ufaransa ambako atakutana na Rais Jacques CHIRAC na hatimae kuzuru Uholanzi. Kabla ya kuanza safari yake, Rais huyo wa Burundi alielezea nia ya kukutana na wajumbe wa Palipehutu-FNL, chama pekee miongoni mwa wapiganaji ambacho bado kinakaidi kusaini mapatano ya kusitisha mapigano na serikali. Mkutano huo unaoitwa kikao cha washirika wa maendeleo wa Burundi, umeandaliwa na Ubelgiji iliyokuwa mkoloni wa Burundi kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).