1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS Uingereza yakabiliwa na shinikizo katika mkutano wa umoja wa Ulaya mjini Brussels

16 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CF2w

Uingereza inakabiliwa na shinikizo kubwa katika mkutano wa kilele wa umoja wa Ulaya mjini Brussels. Viongozi wa umoja huo wanakutana kujaribu kuiokoa katiba mpya ya umoja huo na kumaliza mzozo wa bajeti. Waziri mkuu wa Uingereza bwana Tony Blair, amesema hatakubali kukiachilia kiwango cha euro milioni tano inachokipokea kutoka kwa umoja wa Ulaya kila mwaka.

Rais wa Ufaransa Jacques Chirac amekataa wito wa Blair wa kupunguzwa kwa ruzuku inayotolewa kwa wakulima. Waziri mkuu wa Luxembourg, Jean-Claude Juncker, ambaye ni mwenyekiti katika mkutano huo wa siku mbili, amesema ana wasiwasi ikiwa makubaliano kuhusu bajeti ya mwaka 2007 hadi 2013 yataafikiwa. Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, amesema ikiwa kikao hicho kitashindwa kuutanzua mzozo wa bajeti na kutafuta njia za kuiokoa katiba, umoja wa Ulaya utatumbukia katika mzozo wa kisiasa.

Katiba hiyo ambayo ni lazima iidhinishwe za mataifa yote 25 wanachama, ilikatiliwa na wafaransa na wadachi mwishoni mwa mwezi uliopita. Rais wa Ujerumani, Horst Köhler, alisema hatakamilisha kuidhinishwa kwa katiba hiyo mpaka ifanyiwe marekebisho na mahakama.