1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS-Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya asema hakuna ishara ya kuwepo mjadala mpya wa mapendekezo ya katiba ya Ulaya.

30 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CF8U

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barroso,amesema hakutakuwa na mjadala mpya utakaoanzishwa kuhusiana na mapendekeozo ya katiba ya Umoja wa Ulaya,licha ya raia wa Ufaransa kuikataa katika kura ya maoni waliyopiga jana.

Bwana Barroso amesema serikali za mataifa mengine 24 yaliyowanachama wa Umoja wa Ulaya,hawajaonesha ishara yoyote kuwa wanahitaji kufunguliwa upya kwa ukurasa mpya wa majadiliano juu ya katiba hiyo ambayo imetayarishwa kwa ajili ya kurahisisha upitishwaji wa maamuzi ya umoja huo.

Jana wakati wa kura ya maoni nchini Ufaransa,wapiga kura wa nchi hiyo wanaofikia asilimia 55 waliyakataa mapendekezo ya katiba hiyo,na kuifanya kuwa ni nchi ya awali kupinga kuidhinisha na kuonekana kama wamelitosa jahazi.

Mataifa mengine tisa,ikiwemo Ujerumani tayari yameshaafiki juu ya mapendekezo ya katiba hiyo,lakini hata hivyo katiba hiyo itaweza kufanyakazi tu iwapo mataifa yote 25 wanachama wa Umoja wa Ulaya watakaporidhia.

Raia wa Uholanzi wao wanapiga kura ya maoni keshokutwa siku ya Jumatano na uchunguzi wa hivi karibuni unaonesha wale wanaopinga katiba hiyo wapo wengi nchini humo.