1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Kishindo kizito chakabili mazungumzo ya Umoja wa Ulaya juu ya Uturuki

2 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEVn

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakabiliwa na kishindo kizito leo hii jioni cha Austria juu ya masharti ya kuanza mazungumzo hapo kesho ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya wakati serikali ya Vienna ikidai Uturuki ipewe ushirika wa upendeleo maalum na sio uwanachama kamili.

Rais wa Uturuki Ahmet Necdet Sezer ameliambia bunge mjini Ankara kwamba lengo la kihistoria la Uturuki kujiunga na umoja huo tajiri liko katika njia isioweza kutangulika na amewaonya viongozi wa Umoja wa Ulaya kwamba vikwazo vyovyote vile vipya vitasimamisha ukuta wa chuki isio na msingi na kukwamisha maendeleo ya Ulaya.

Hata hivyo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Havier Solana ana imani kwamba makubaliano bado yanaweza kufikiwa kwa mazungumzo hayo ya kesho ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.Hata hivyo katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag Solana amesisitiza kwamba mazungumzo hayo pekee sio hakikisho kwamba Uturuki itaruhusiwa kujiunga na umoja huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Abdullah Gul mwenye wasi wasi amemwambia waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw ambaye atakuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa Umoja wa Ulaya kwamba hatokwenda Luxembourg hadi hapo atakapoona kile kilichoagizwa kuzungumzwa kimesainiwa na nchi wanachama 25 wa Umoja wa Ulaya.