1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit hadi Januari 31, 2020

28 Oktoba 2019

Umoja wa Ulaya umekubaliana kusogeza mbele muda wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya hadi Januari 31 mwaka 2020, makubaliano yaliyofikiwa siku tatu tu kabla ya kufikia mwisho wa muda wa awali wa Brexit.

https://p.dw.com/p/3S6RW
Großbritannien Brexit Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Baada ya mazungumzo mafupi ya wanadiplomasia mjini Brussels, rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk aliandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba mataifa 27 yaliyosalia yatakubaliana na ombi la Uingereza la kuongezewa muda wa kile alichokitaja kama Flextension, inayomaanisha Uingereza inaweza kuondoka hata kabla ya muda huo waliokubaliana, iwapo makubaliano kati ya Ulaya na Uingereza yataridhiwa na bunge la taifa hilo.

Mjini London, msemaji wa waziri wa Uingereza Boris Johnson James Slack amewatupia wabunge wa Uingereza lawama akisema ndio waliosababisha muda huo kusogezwa mbele.

Johnson hivi sasa anajiandaa kuomba kuitishwa uchaguzi mpya akiangazia kupata bunge litakalounga mkono makubaliano yake, lakini huenda pia akaukosa huo uungaji mkono anaoutafuta. Wabunge wanakutana baadae hii leo kujadili ombi hilo la Johnson.

DW-Karikatur von Sergey Elkin - Brexit-Pläne von Boris Johnson
Kikaragosi kikimuonyesha waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiomba msaada

Wachumi wanasema hatua hiyo ya Ulaya ni bora kuliko ya Brexit bila ya makubaliano ambayo ingeathiri uchumi si tu kwa Uingereza bali pia Ulaya, kama Tony Travers, mchambuzi kutoka chuo cha uchumi cha London anavyosema, "Serikali mara zote imesema iko tayari kutoka bila ya makubaliano. Ukweli ni kwamba kama kusingefikiwa makubaliano, isingekuwa mwisho wa Brexit, na badala yake ingekuwa ndio mwanzo wa Uingereza kuanzisha mazungumzo mapya ya kimahusiano sio tu Umoja wa Ulaya, lakini pia Marekani na mataifa mengine mengi kwa sababu wangetakiwa kuwa na makubaliano mapya ya biashara."

Kulingana na Tusk, uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuwekwa rasmi kimaandishi, hii ikimaanisha kuwa mkutano maalumu wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya huenda usiwe wa lazima katika kuridhia hatua hiyo.

Akizungumza kwa masharti ya kutotambulishwa, mwanadiplomasia mmoja ameliambia  shirika la habari la AP kwamba makubaliano yaliyopo hayatajadiliwa upya katika kipindi hicho kilichoongezwa.

Sheria mpya iliyopitishwa na bunge la Uingereza inamlazimisha Johnson kuomba kuongezwa muda, kitu ambacho hakukitaka.

Ujerumani imekaribisha uamuzi huo wa kusogezwa mbele muda wa Brexit. Msemaji wa kansela Angela Merkel, Steffen Seibert amesema ni suluhu nzuri lakini pia akisifu mataifa wanachama kuonyesha mshikamano.