1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil na Argentina kupambana Jumatano

1 Julai 2019

Ulimwengu wa soka utasimama Jumatano pale watani wa jadi Brazil na Argentina watakapokuwa wanakwaana katika nusu fainali ya taji la kuwania ubingwa wa Amerika Kusini Copa America.

https://p.dw.com/p/3LPy5
Fußball Argentinien vs Brasilien | Neymar
Picha: Getty Images/AFP

Cheche kutoka pande zote tayari zimeanza kurushwa kuelekea mchuano huo wa kukata na shoka.

Mshambuliaji wa Brazil Gabriel Jesus anasema Argentina watakuwa na wakati mgumu kuivunja safu yao ya ukabaji kwa kuwa katika mechi nne walizocheza hawajakubali goli langoni mwao.

Lakini kuna jina moja ambalo liko akilini mwa beki wa kati wa Brazil Thiago Silva, Lionel Messi. Silva anakiri kwamba ni atakuwa na wakati mgumu kucheza dhidi ya nyota huyo.

"Kwangu mimi Messi ndiye mchezaji bora katika historia, mchezaji bora ambaye nimewahi kumuona. Ni fahari kubwa kupambana naye. Lakini kwa sasa ni Brazil na Argentina, nitajaribu kuitetea timu yangu na tutafurahia baadae baada ya kupita," Silva.

Silva ameendelea kusema kuwa ni vigumu sana kumzuia Messi asionyeshe mchezo mzuri katika mechi.

"Kila wakati ambapo nimepembana naye, iwe katika timu ya taifa au katika ngazi ya klabu kwenye Champions League, ni vigumu sana kumzuia. Hata ukausoma mchezo wake vipi, utashangazwa tu na uwezo wake, siku zote ataleta tofauti mchezoni," alisema Silva.

Iwapo Argentina watafuzu kwenye fainali na kushinda basi watakuwa wameifikia rekodi ya Uruguay ya kushinda mataji 15 ya mashindano hayo ya Copa America.