1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson akabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye

6 Juni 2022

Chama tawala cha Kihafidhina nchini Uingereza kitafanya kura ya kutokuwa na imani baadae leo ambayo huenda ikamuondoa madarakani Waziri Mkuu Boris Johnson.

https://p.dw.com/p/4CKOC
Großbritannien Premierminister Boris Johnson
Picha: Matt Dunham/AP Photo/picture alliance

Uongozi wa Johnson ambaye amekumbwa na kunusirka na misukosuko mara kadhaa umekuwa ukitiliwa shaka kwa miezi sasa.

Iwapo Johnson atapoteza kura hiyo ya kutokuwa na imani naye itakayopigwa na wabunge 359 wa chama chake cha Kihafidhina, basi chama hicho kitachagua kiongozi mwengine ambaye atauchukua wadhfa wa Waziri Mkuu pia. Kulingana na sheria za sasa za chama hicho, iwapo atashinda kura hiyo basi ataendelea na uongozi wake na hatokabiliwa na pingamizi kwa mwaka mmoja mzima.

Msemaji wa afisi ya waziri huyo mkuu amesema kura hiyo ni "fursa ya kutilia kikomo miezi kadhaa ya uvumi na kutoa nafasi kwa serikali kuendelea na kazi yake ya kuwatimizia raia vipau mbele vyao."

Johnson afahamishwa kuhusiana na kura ya kutokuwa na imani naye

Kwa kura hiyo kufanyika ni sharti asilimia 15 ya wabunge wa chama hicho wawasilishe maombi kwa mkuu wa chama na mwenyekiti wa chama hicho cha Kihafidhina Graham Brady amethibitisha kupokea barua za kutosha kuweza kuanzisha mchakato huo wa kura ya kutokuwa na imani. Brady hakutaja idadi kamili ya barua alizopokea akisema wabunge wengine walitaka barua zao zifike baada ya sherehe za kuadhimisha miaka 70 ya malkia Elizabeth kuwa uongozini.

Großbritannien Premierminister Boris Johnson
Boris Johnson akijitetea bungeniPicha: PRU/AFP

Brady vile vile amesema kuwa Johnson alifahamishwa usiku wa jana kuhusiana na kufanyika kwa kura hiyo ya kutokuwa na imani naye.

Waziri Mkuu Johnson amenusurika kadhia nyingi za kisiasa ila kwa miezi kadhaa sasa ameshindwa kulisafisha jina lake kutokana na kashfa kadhaa za kimaadili zinazomkabili. Kubwa zaidi ya kadhia hizo ni ile ya uvunjaji sheria za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona ambapo kuliandaliwa sherehe kadhaa za unywaji pombe katika afisi za serikali. Sakata hiyo iliyoitwa "Partygate scandal" ilizua ghadhabu miongoni mwa Waingereza.

Mwezi uliopita ripoti ya mchunguzi wa utumishi wa umma Sue Gray ilisema uongozi wa nchi hiyo ndio unaostahili kuchukua jukumu la sherehe hizo za unywaji pombe zilizofanyika katika afisi ya waziri mkuu wakati ambapo Uingereza ilikuwa chini ya vikwazo vikali vilivyozuia mikusanyiko na hata watu kuwatembelea jamaa zao waliokuwa wanafariki kutokana na Covid mahospitalini.

Wahafidhina wanaamini hawaezi kushinda uchaguzi ujao na Johnson uongozini

Waziri Mkuu Johnson wakati huo alisema kwamba anachukua jukumu la yote yaliyofanyika ila akakata kujiuzulu akiwataka Waingereza wayasahau yaliyotokea na watazame masuala ya kuufufua uchumi na vita vya Ukraine.

UK | Großbritannien | London | Protest gegen Lockdown Parties
Maandamano ya kumtaka johnson ajiuzulu mjini LondonPicha: imago images/ZUMA Wire/Vuk Valcic

Umaarufu wa Johnson umeshuka kwa kiwango kikubwa miongoni mwa Wahafidhina katika siku za hivi karibuni na wabunge wengi wa chama chake wamejitokeza na kusema hawaamini iwapo chama chao kinaweza kushinda uchaguzi mkuu ujao chini ya uongozi wa Johnson.

kura za maoni zimeonyesha Waingereza wengi kutokubaliana na uongozi wake wakisema Johnson alidanganya peupe kuhusiana na sakata hiyo ya "Partygate" na anastahili kujiuzulu.

Chanzo: AFPE/AP