1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bondia Khelif aomba kukomeshwa uonevu dhidi ya wanamichezo

5 Agosti 2024

Bondia wa Olimpiki Imane Khelif amesema wimbi la ukosoaji wa chuki alilokabiliana nalo kuhusiana na dhana potofu kuhusu jinsia yake linaathiri heshima ya binaadam.

https://p.dw.com/p/4j8UJ
Bondia mwanamke Imane Khelif katika Michezo ya Olimpiki Paris 2024
Ametoa wito wa kukomeshwa tabia ya uonevu dhidi ya wanamichezo baada ya dhana potofu kuhusu jinsia yakePicha: Ciro Fusco/ANSA/picture alliance

Ametoa wito wa kukomeshwa tabia ya uonevu dhidi ya wanamichezo baada ya kuathirika pakubwa na upinzani wa kimataifa dhidi yake. "Ninatuma ujumbe kwa watu wote wa dunia kuzingatia kanuni za Olimpiki, kwa mujibu wa Mkataba wa Olimpiki, kujiepusha kuwaonea wanamichezo wote kwa sababu jambo hili lina madhara, madhara makubwa. Linaweza kuharibu Maisha ya watu, linaweza kuua mawazo ya watu, nafsi na akili, Na inaweza kuwagawanya watu."

Soma pia: Olimpiki Paris 2024: Wanariadha wa Afrika wang´ara

Khelif pia alitoa shukrani kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki na rais wake, Thomas Bach, kwa kusimama naye wakati bodi ya zamani iliyopigwa marufuku ya ndondi ya Olimpiki ilizua ghasia kuhusu ushiriki wake huko Paris.

Mualgeira Khelif tayari ameshinda medali yake ya kwanza ya Olimpiki kwa ushindi mara mbili mjini Paris wakati kukiwa na miito ya kutaka aondolewe katika Michezo hiyo kwa misingi ya dhana potofu kuhusu jinsia yake. Atapanda tena ulingoni kesho Jumanne katika ndondi kitengo cha kilo 66 kwa wanawake nusu fainali. Ushindi wa Khelif na bondia mwenzake Lin Yu-ting wa Taipei ya China ulingoni mjini Paris umekuwa moja ya hadithi kubwa za Olimpiki.

afp, dpa, reuters, ap