1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine avutana na tume ya uchaguzi huko Uganda

15 Desemba 2020

Mgombea mkuu wa upinzani kwenye uchaguzi wa urais nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, ametofautiana na tume ya uchaguzi kwa madai kwamba yeye na mwenzake wa chama cha FDC wanakiuka mwongozo wa kampeni.

https://p.dw.com/p/3ml15
Robert Kyagulanyi
Picha: Emmanuel Lubega/DW

Badala yake ameitaka tume hiyo kujiuzulu kwa kushindwa kudhibiti majeshi na polisi wanaowahangaisha. Wakati huohuo, serikali ya Ugandaimeandikia makampuni ya mitandao ya kijamii google, facebook na youtube kuyaondoa majukwaa ya vyombo vya habari vinavyorusha moja kwa moja kampeni za mgombea urais Robert Kyagulanyi. 

Wagombea urais  Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine pamoja na Patrick Oboi Amuriat wamefika mbele ya tume ya uchaguzi kuitikia mwito wa kuwataka kujieleza kuhusu mienendo yao ya kukiuka mwongozo wa kampeni pale wanapoendesha mikutano ya hadhara na kuwatia wafuasi wao katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19.

Lakini wagombea hao wanalalamika kuwa vyombo vya usalama vinatumia  nguvu za kupindukia kwa kisingizio cha kudhibiti ugonjwa huo. Aidha Bobi Wine ameshtumu tume hiyo kwa kumpendelea Rais Museveni na kuitaka ijiuzulu kwa kushindwa kusimamia kampeni zao ipasavyo.

Kwingineko, serikali ya Uganda kupitia tume ya mawasiliano UCC inayataka makampuni ya kimataifa ya Google, Facebook na Youtube kusimamisha vyombo vya habari vya mitandaoni vinavyorusha habari za moja kwa moja za kampeni za Bobi Wine.Mamlaka ya mawasiliano ya Uganda inadai kuwa vyombo hivyo vinatumiwa kuchochea ghasia na machafuko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Bildkombo Yoweri Museveni und Bobi Wine
Rais Museveni na mpinzani wake mkuu Bobi Wine

Kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa makao makuu ya kampuni za Google, Facebook, na Youtube, Tume ya Mawasiliano ya Uganda, UCC, imeorodhesha idhaa za mitandaoni 13 ambazo inataja kukiuka  kanuni za mawasiliano si tu za Uganda lakini pia za kimataifa pale zinaporushwa habari zinazochochea chuki za vurugu za kisiasa. Tume hiyo imefafanua kuwa taasisi ya polisi kupitia kwa wizara ya masuala ya ndani na pia kurugenzi la usalama wa kitaifa  zimetoa malalamiko kuhusu mienendo hiyo ambayo inasemekana ilisababisha vifo vya watu 54 mwezi uliyopita.

Afrika | Kenia Uganda Proteste  Bobi Wine Opposition
Wafuasi wa mgombea urais wa Uganda Bobi WinePicha: AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wameikosoa tume hiyo kwa kutuma ombi ambalo linadhihirisha kuwa kuna mambo ambayo hayaendi sawa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Lakini wanaharakati wa haki za binadamu wanapinga hatua hiyo wakisema kuwa inakiuka haki ya binadamu na kwamba serikali inahofia vyombo hivyo vinajulisha ulimwengu ukweli ka mambo nchini Uganda. 

Watu kiasi 28 wauwawa Uganda

Wanaharakati wana imani kuwa makampuni hayo ya kimataifa hayataitikia ombi la serikali ya Uganda kwani katika enzi hii yanachangia pakubwa katika kulinda haki za binadamu. Lakini wanahofia kuwa makampuni ya mawasiliano nchini Uganda yatashurutishwa kuzuia majukwaa hayo kuendesha shughuli zake. Sarah Kihika ni mwanaharakati wa shirika la Chapter 4.

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa limekataza wafanyakazi wake kufanya safari kuja Uganda kwa kuhofia usalama wao. Hatua hii imeleta wasiwasi kwamba hata mataifa mengine ya kigeni yatachukua maamuzi kama hayo na kwa hiyo kuathiri uchumi wa Uganda ambao ndiyo mwanzo umekuwa ukiboreka katika kipindi cha miezi mitatu hivi. Mwanasheria Nicholas Opiyo amehimiza serikali kuondoa dhana hizi kwamba Uganda si salama kwa sasa kwa kuhakikisha kuwa majeshi na polisi yanajiepusha na vitendo vya kuwahujuma raia.