1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken asema Marekani itaendelea kuisaidia Ukraine

16 Januari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema Washington itaendelea kuiunga mkono Ukraine baada ya kufanya mkutano na Rais Volodymyr Zelensky.

https://p.dw.com/p/4bKND
Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Kauli ya Blinken ameitoa licha ya mvutano katika bunge la Marekani kuhusu uidhinishaji wa msaada mpya kwa Ukraine.

"Nataka kuanza kwa kuwasilisha ujumbe wa Rais Biden wa uungwaji mkono wa dhati kwa Ukraine. Hii inatokea wakati unaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya karibu kila siku kutoka kwa Urusi yanayolenga miundombinu na raia. Tunaona hayo kila siku, lakini pia tunaona ujasiri mkubwa wa watu wa Ukraine."

Wakiwa katika kongamano la kiuchumi la dunia mjini Davos Uswisi, mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameeleza matumaini yake kuwa washirika wao wa Ulaya pia wataiunga mkono Ukraine.

Zelensky kuizuru Uswisi kuimarisha uungaji mkono wa kimataifa

Naye mshauri wa usalama wa taifa wa Rais Joe Biden, Jake Sullivan, pia amemwambia Zelensky kwamba Marekani na washirika wake wamedhamiria kuhakikisha kuwa, Urusi inafeli na Ukraine inapata ushindi.

Zelensky ambaye anahudhuria kongamano hilo kwa mara ya kwanza kama rais, baada ya kulihutubia kwa njia ya video katika miaka ya nyuma, ametoa shukrani kwa utawala wa Biden na "msaada wa pande mbili" katika bunge la Marekani.

Maafisa wakuu wa Marekani, Umoja wa Ulaya, China, Mashariki na Kati na sehemu nyingine duniani wanahudhuria kongamano hilo.