1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aona fursa kwa Israel kushirikishwa kikanda

9 Januari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameiambia Israel baada ya kuyatembelea mataifa ya Kiarabu kwamba ameona fursa kwake kujenga uhusiano wa karibu katika kanda ya Mashariki ya Kati baada ya mzozo wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4b1Jl
Israel Tel Aviv | Antony Blinken akutana na Isaac Herzog
Waziri Antony Blinken akifanya mazungumzo na Rais wa Israel, Isaac HerzogPicha: Abir Sultan/AFP/Getty Images

 Akiwa kwenye misheni inayolenga kuzuwia mzozo wa Israel na Hamas kusambaa na kuwa vita vya kikandaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema Saudi Arabia, Jordan, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu na Uturuki, zitazingatia kushiriki katika ujenzi mpya na utawala wa Gaza, jambo ambalo mataifa hayo yamekuwa yakisita kuahidi kabla ya kusitishwa kwa mapigano.

Lakini Marekani na Israel zinasalia na tofauti kubwa kuhusu usimamizi wa Gaza baada ya watawala wa sasa Hamas kushindwa. Maafisa wa Marekani wanataka Mamlaka ya Palestina, ambayo kwa sasa inatawala baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, kuchukua uongozi wa Gaza na mazungumzo yaanze tena kuhusu kuundwa kwa taifa la Palestina. Viongozi wa Israel wamepinga vikali mapendekezo yote mawili.

Soma pia: Blinken ziarani Mashariki ya Kati katika juhudi za kumaliza vita vya Gaza

Blinken pia anajaribu kuzuia mzozo huo usienee baada ya kuongezeka kwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah na vitisho vya Israel kuongeza hatua za kijeshi ili kukomesha mashambulizi ya karibu kila siku ya kuvuka mpaka kutoka Lebanon, yanayofanywa na kundi hilo la wanamgambo.

Israel Tel Aviv | Kuwasili kwa waziri wa nje wa Marekani Antony Blinken
Blinken amesema mataifa ya kanda ya MAshariki ya KAti yako tayari kushirikiana na Israel ikiwa kutakuwa na ahadi ya kweli kuhusu kuundwa kwa taifa la Palestina.Picha: Evelyn Hockstein/Pool/AP/picture alliance

Marekani inaishinikiza Israel kupunguza mashambulizi yake Gaza na kuendesha operesheni za kuwalenga kwa usahihi wapiganaji wa Hamas. Lakini kasi ya vifo na uharibifu imesalia sawa, huku maafisa wa Gaza wakiendelea kuripoti vya mamia ya Wapalestina kila siku.

Israel imeapa kuendeleza kampeni yake hadi itakapoiangamiza Hamas katika Ukanda wote wa Gaza, kujibu shambulio la Oktoba 7 ambamo wapiganaji wa kundi waliwauwa takriban watu 1,200, hasa raia, kusini mwa Israeli na kuwachukuwa mateka wengine karibu 250.

Mambo bado magumu kwa Israel

Hata hivyo miezi mitatu tangu kuanza kwa operesheni yake ya kijeshi, Hamas imeendelea kutoa upinzani mkali, licha ya jeshi la Israel kusema limeharibu miundombinu yake kaskazini mwa Gaza, ambako maeneo makubwa yameharibiwa, na mapigano pia bado yanaendelea huko. Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari aliarifu kuwa vita hivyo vitaendelea katika mwaka wote wa 2024.

Soma pia: Marekani imetilia shaka juhudi zinazofanywa na Israel za kuwalinda raia

Tangu vita kuanza, mashambulizi ya Israel Gaza yameua zaidi ya Wapalestina 23,000, karibu theluthi mbili yao wakiwa wanawake na watoto, na zaidi ya 58,000 wamejeruhiwa, kulingana na Wizara ya Afya ya  Gaza inayoendeshwa na Hamas. Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kadhaa yanaiorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Uturuki I Waziri Antony Blinken azuru Uturuki
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akikutana na Waziri Blinken na ujumbe wake mjini Istanbul, Januari 6, 2024.Picha: Murat Cetinmuhurdar/Turkish Presidency/Anadolu/picture alliance

Ofisi ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, imesema kuwa mashambulizi ya Israel katika eneo la kati na kusini mwa Gaza yamekuwa na "matokeo mabaya," na kusababisha vifo vya raia, kupunguzwa kwa shughuli za misaada katika eneo la kati na kuhatarisha kufungwa kwa hospitali kuu tatu.

Mzozo huo pia unatishia kutanuka majibizano kati ya Israel na Hezbollah. Hii leo Hezbollah imesema imefanya shambulio la droni dhidi ya Israel kujibu mauaji ya vikosi vya Israel dhidi ya kamanda wake wa juu nchini Lebanon. Jeshi la Israel limekiri kushambuliwa kwa kambi yake ya kaskazini, lakini limesema hakukuwa na uharibifu wala vifo.