1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yaunga mkono Sweden kujiunga na NATO

31 Mei 2023

Marekani imeitolea mwito Uturuki kuidhinisha ombi la Sweden kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO huku Waziri wa mambo ya nje Antony Blinken akisema "wakati ni sasa" kwa nchi hiyo ya Nordic kujiunga na jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/4RzKq
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken(kushoto) akiwa na waziri mkuu wa Sweden, Ulf Kristersson, alipokuwa ziarani nchini humo, 30.05.2023
Picha: Jonas Ekströmer/TT News Agency/AP/dpa/picture alliance

Blinken ameongeza kuwa utawala wa Rais Joe Biden unaamini kuwa Uturuki inapaswa kuuziwa ndege za kivita za kisasa aina ya F-16 haraka iwezekanavyo. 

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson mjini Lulea, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amesema Sweden imetimiza vigezo vyote vya kujiunga na NATO kutoka siku ya kwanza na kwamba nchi hiyo imekwenda mbali zaidi na kushughulikia wasiwasi uliotolewa na Uturuki.

"Sisi pamoja na washirika wetu tumejitolea kuisaidia Sweden kushughulikia mahitaji yake ya kiusalama, bila kujali iwapo ombi lao litaidhinishwa kesho au baada ya wiki chache zijazo. Tumeweka wazi kwamba hatotovumilia uchokozi wowote dhidi ya Sweden, bila kujali hadhi yake."

Blinken aidha amesisitiza kuwa suala la Sweden kujiunga na NATO halina uhusiano wowote na Uturuki kuuziwa ndege za kivita za Marekani, japo amekiri kuwa baadhi ya wabunge wa Marekani wanahisi masuala hayo yana uhusiano wa moja kwa moja.

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani pia amemueleza Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu juu ya utayari wa Sweden kujiunga na jumuiya hiyo.

Soma pia: Von der Leyen kuwania ukuu wa NATO

Sweden na Finland zilituma maombi ya kuwa wanachama wa NATO mwaka jana, na kuachana na sera ya muda mrefu ya kutoegemea upande wowote wa kijeshi kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Kimsingi, maombi ya kujiunga na NATO ni lazima yaidhinishwe na nchi wanachama wote.

Jumuiya hiyo inayoongozwa na Marekani, ina makubaliano ya pamoja ya ulinzi ikimaanisha kuwa shambulio dhidi ya mwanachama mmoja, linatafsiriwa kama shambulio kwa nchi wanachama wote.

Finland ilijiunga rasmi na jumuiya hiyo mwezi uliopita japo ombi la Sweden bado linasubiri kuidhinishwa.

Sweden yaishukuru Marekani kwa kuiunga mkono

Deutschland Schweden Premierminister Ulf Kristersson Olaf Scholz
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf KristerssonPicha: ANNEGRET HILSE/REUTERS

Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson amesema, "Natoa shukrani za dhati kwa uungwaji mkono wa Marekani kwa Sweden kujiunga na NATO. Hiyo ina maana kubwa kwetu. Tumetuma ombi la uanachama kwa sababu tunatambua umuhimu wa kutetea uhuru na demokrasia. Lakini pia, tunataka kuleta uwezo wetu kwa lengo moja. Kama mwanachama, Sweden itakuwa nguzo muhimu ya usalama kwa jumuiya nzima."

Hungary na Uturuki ndio wanachama pekee wa NATO ambao bado hawajaidhinisha ombi la Sweden ingawa Ankara inaonekana kuwa kizingiti kikuu. Hii ni kutokana na hatua ya Uturuki kuishtumu Sweden kwa kuwahifadhi wanachama wa chama cha wafanyikazi wa Kikurdi PKK, ambacho kinachukuliwa na Uturuki kama "kundi la kigaidi."

Soma pia: Finland kujiunga rasmi na NATO siku ya Jumanne

Maandamano ya chuki dhidi ya uislamu yaliyofanyika mjini Stockholm mwezi Januari na kuchomwa kwa Quran pia kulitia doa uhusiano kati ya Sweden na Uturuki.

Mnamo mwezi Juni mwaka uliopita, Uturuki, Sweden na Finland zilitia saini kile kinachojulikana kama "mkataba wa pande tatu" ili kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na Uturuki kuhusu makundi yaliyopigwa marufuku.

Hata hivyo, Uturuki inailaumu Sweden kwa kutotimiza ahadi zake katika mkataba huo wa pande tatu.

Blinken yuko nchini Sweden kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa baraza la biashara na teknolojia la Marekani na Ulaya, na anatarajiwa kusafiri hadi Oslo Norway leo Jumatano kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO kabla ya kufanya ziara kwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo Finland mnamo siku ya Ijumaa.